Bila ardhi ya makazi mafuriko yataendelea kutuangamiza

14May 2017
Mwinyi Sadallah
Nipashe Jumapili
Bila ardhi ya makazi mafuriko yataendelea kutuangamiza

IDADI ya watu Zanzibar inaendelea kuongezeka huku tatizo la makazi likitikisa na kulazimisha baadhi ya wananchi kujenga nyumba bila kuzingatia sheria za mipango Miji Visiwani hapo.

Kwa mujibu wa ripoti ya sensa ya idadi ya watu na makazi ya mwaka 2012 imebainisha kuwa Zanzibar idadi ya watu ni zaidi ya milioni 1.4. Katika visiwani vya Unguja na Pemba, kote tatizo la makazi linaonekana kukua na kuzidi kuwa changamoto kubwa.

Wananchi wa pande zote wanatatizwa na nyumba duni, ujenzi mabondeni na maeneo hatarishi, linalochangiwa na sababu mbalimbali ikiwamo umaskini, urasimu wa upatikanaji wa viwanja kwa ajili ya ujenzi wa makazi, kutokufanikiwa.

Tatizo la makazi limeanza kuleta madhara makubwa kwa wananchi kutokana na kulazimika kujenga mabondeni na sehemu za mikondo ya kupitisha majitaka na kusababisha familia nyingi kuathirika na mafuriko kila mvua zinaponyesha.

Pamoja na familia kuumizwa majengo ya shule yanageuzwa kambi za waathirika wa mafuriko huku wanafunzi wakipumzika kusoma.

Urasimu wa upatikanaji wa viwanja vya ujenzi wa nyumba za makazi kimekuwa kilio cha miaka mingi na kusababisha baadhi ya wananchi maombi yao kukaa kwenye mamlaka zinazohusika hata zaidi ya miaka 20.

Nyaraka hizo zinarundikwa bila ya kushughulikiwa , urasimu huo na kujengeka kwa mazingira ya kutaka kutoa chochote, yamekuwa chanzo cha ujenzi wa nyumba katika maeneo yasiyokuwa salama.

Tukumbuke madhara ya mafuriko yanachangia kuongezeka umaskini kwa wananchi wanaoathirika na kurudisha nyuma mpango wa serikali wa kukuza uchumi na kupunguza umaskini .

Ripoti ya awali ya athari za mafuriko yaliyotokea tangu kuanza kunyesha mvua za masika,inayotolewa na Mamlaka ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar , imeleeza kuwa nyumba 992 zimeathirika zikiwamo 667 kisiwani Unguja na 325 Pemba pamoja na mtoto kupoteza maisha baada ya kuangukiwa na ukuta.

Ujenzi holela umesababisha mikondo ya maji kupoteza mwelekeo na kuathiri miundombinu ya barabara ikiwamo kubomoka kwa madaraja na kusababisha hasara kwa serikali kwa vile fedha nyingi za umma zinatumika kuimarisha miundo miundo.

Wakati umefika kwa viongozi kusimamia sheria kwa vitendo haiwezekani watu kujenga katika mito, mikondo ya maji au katika vyazo vya maji na ujenzi kufanyika mpaka kumalizika bila ya wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria pamoja na watendaji kulipwa mishahara kila mwezi.

Katika kuondoa tatizo la ujenzi usiozingatia mipango miji serikali kuondosha urasimu katika upatikanaji wa viwanja vya ujenzi wa nyumba za makazi kwa wananchi hasa wanyoge.

Kama mtu analazimika kukaa akisubiri kupatiwa kiwanja robo karne bila ya mafanikio ndiyo chanzo kwa wananchi wengine kuamua kuvamia mabondeni, katika mikondo ya mito na bahari na kujenga ili kujipatia hifadhi na familia zao.

Uzazi wa mpango kwa Zanzibar ni jambo la kuzingatia . Serikali inawajibika kutumia juhudi zaidi kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya uzazi usio na mpango, kunakoongeza idadi kubwa ya watu wasiolingana na huduma za kijamii na ukuaji wa uchumi.

Mazoea ya mtu mmoja kuwa na wake watatu hadi wanne na kuzaa hata watoto 30 pia unahitaji kuangaliwa kwa makini kama serikali imekusudia kufanikisha mpango wa uzazi salama.

Hatua ya wafanyabiashara na mifuko ya maendeleo kujitokeza kujenga nyumba za biashara makazi ni ya kushangiliwa lakini suala la bei litizamwe kwa jicho la pili ili wateja wanaonunua wawe watu wa kipato cha chini wanaokimbilia kuishi mabondeni.

Mafuriko yanayotokea Zanzibar na kuathirika nyumba nyingi Zanzibar lazima iwe fundisho kwa wanaosimamia ardhi kwa kuhakikisha kuwa urasimu wa upatikanaji viwanja unaondoka na kuwanufaisha wananchi wanyonge.

Kama mfumo wa ugawaji wa viwanja kipaumbele kikubwa kitawekwa kwa wananchi wa chini tatizo la watu kuvamia maeneo hatarishi na kujenga makazi litapungua kwa kiwango kikubwa au kubakia historia.

Lakini hatua ya Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, kuanzisha Shirika la Nyumba Zanzibar umekuja kwa wakati muafaka kutokana na tatizo la makazi na ogezeko la idadi ya watu.

Hatua ya kuanzisha shirika pia ni kuenzi kwa vitendo sera ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar Sheikh Abeid Amani Karume, ya kuwapatia makazi bora wananchi wake iliyoasisiwa baada ya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964.

Ghorofa zilizojengwa katika Visiwa vya Unguja na Pemba zilikuwa kielelezo cha msingi katika matumizi bora ya ardhi hasa kwa kuzingatia kuwa rasilimali hiyo kwa Zanzibar ni ndogo na watu wanaendelea kuongezeka.

Habari Kubwa