Taarifa za teknolojia zilizogonga vichwa vya habari mwaka 2017-1

02Jan 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
  Taarifa za teknolojia zilizogonga vichwa vya habari mwaka 2017-1

UTAFITI ambao unafanyia majaribio teknolojia inayodaiwa kuwa na uwezo wa kutofautisha watu wapenzi wa kawaida na wale wa jinsia moja umezua mzozo mkali kati ya waliotayarisha teknolojia hiyo na watetezi wa haki za wapenzi wa jinsia moja.

TEKNOLOJIA INAYOWATAMBUA WAPENZI WA JINSIA MOJA

 

Watafiti hao kutoka Chuo Kikuu cha Stanford nchini Marekani, wanadai kwamba wameunda programu ya kompyuta ambayo inaweza kuangalia uso wa mtu na maumbile yake na kutofautisha kati ya wapenzi wa jinsia moja na wapenzi wengine.

Programu hiyo inaweza kutambua mambo ambayo mtu wa kawaida hawezi kuyabaini, wanasema.

Lakini watetezi wa haki za mashoga wameshutumu utafiti huo na kuuita kuwa ni ‘hatari’ na kwamba ni ‘sayansi isiyo na manufaa.’

Hata hivyo, wanasayansi wahusika wamesema wanaiopinga programu hiyo, hawajaielewa vyema.

Maelezo ya kina kuhusu mradi huo yatachapishwa katika jarida moja kuhusu sifa za watu na saikolojia ya kijamii.

GARI LA MWENDO KASI ZAIDI DUNIANI LAANZA MAJARIBIO

Gari lililoundwa nchini Uingereza linaloweza kwenda kwa kasi ya kilomita 1,610 kwa saa, linafanyiwa majaribio yake ya kwanza huko Cornwall.

Gari hiyo aina ya Bloodhound SSC linafanya majaribio ya mwendo kasi wa chini wa hadi kilomita 320 kwa saa kwenye uwanja wa ndege wa Newquay.

Likiendeshwa na dereva Andy Green, gari hilo linalenga kuvunja rekodi ya dunia ya mwendo wa kasi zaidi ardhini.

Jaribio hilo litafanywa kwenye barabara maalum iliyojengwa eneo la Nothern Cape nchini Afrika Kusini.

“Tumeunda gari lisilo la kawaida kabisa, lenye uwezo mkubwa na kasi ya juu zaidi katika historia,” Andy Green aliiambia BBC.

L’OREAL KUTUMIA 3D

KUUNDA NYWELE

Kampuni moja nchini Ufaransa imesema kwamba teknolojia sawa na ile inayotumiwa kupiga chapa vitu vya uhalisia, 3D, huenda ikatumiwa kuunda nywele za binadamu na hivyo kuvaa watu wenye vipara.

Itawafaa kwa sababu nywele zitakazoundwa zinaweza kupandikizwa baadaye kwa watu waliopoteza nywele.

Kampuni ya L'Oreal inashirikiana na kampuni ya kupiga chapa viumbe hai ya Poietis, ambayo imeunda teknolojia ya kupiga chapa kwa kutumia laser ambayo inaweza kuunda sehemu za seli za viumbe.

Vinyweleo vya nywele havijawahi kuundwa kwa njia hii awali lakini kampuni hizo mbili zinatarajia kwamba zitaweza kustawisha teknolojia na kuwezesha kuundwa kwa vinyweleo hivyo katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Hata hivyo, shirika moja linalofuatilia watu wanaopoteza nywele limesema bado ni mapema mno kwa watu kuanza kushangilia.

L'Oreal tayari hutumia ngozi iliyoundwa kwa teknolojia ya 3D kufanyia utafiti bidhaa za kutumiwa kwenye ngozi.

NISSAN YAZINDUA KITI CHA

GARI KINACHOTAMBUA JASHO

Kampuni ya magari ya Nissan imezindua kiti cha gari chenye uwezo wa kutambua jasho la binadamu ambacho kampuni hiyo inasema kuwa kitasaidia kupunguza ajali za barabarani.

Teknolojia hiyo inayojulikana kama Soak, hubadilisha rangi ikiwa itatambua kuwa dereva atakuwa ameishiwa maji mwilini.

Utafiti wa awali uliofanywa na taasisi za European Hydration Institute na Loughborough University uligundua kuwa madereva wanaoishiwa maji mwilini huwa na makosa mengi sawa na madereva walevi.

Ngozi hiyo ya kiti iliyoundwa na kampuni moja nchini Uholanzi pia itawekwa kwenye usukani wa gari na viti vya mbele vya gari.

“Hii ni sehemu ya mpango mzima ambao sio tu ni wa kufuatilia gari, bali pia kumfuatilia dereva,” anasema Prof. Peter Wells ambaye ni mmoja wa watafiti.

TEKNOLOJIA YA KUWASAIDIA WAKULIMA WA MIWA

Idadi kubwa ya wakazi wa wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro wanajulikana kwa ukulima hasa wa zao la mpunga na miwa kwa ajili ya kujipatia kipato cha kujikimu kimaisha.

Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni, baadhi ya wakulima hawa walianza kukata tamaa ya ukulima huku wengine wakijaribu kufanya shughuli mbadala kama vile kujiingiza katika biashara ndogo ndogo.

Hii ni baada ya mbegu za miwa walizokuwa wakitumia kupoteza ubora wake, na matokeo yake kushindwa kustahamili mabadiliko ya tabia nchi na hatimaye kuvamiwa na magonjwa.

Masoud Mohamed Mshame ambaye ni mkulima wa miwa kutoka wilayani humo anakiri kwamba kila mwaka, mavuno yalikuwa yakipungua.

“Kulingana na mabadiliko ya hali ya hewa, mwaka jana na mwaka juzi, tulivuna mapato ya chini tofauti na kipato tulichokuwa tunategemea siku za nyuma. Kwa miaka mitatu iliyopita, tulikuwa tunavuna kuanzia tani 30. Ilipofika mwaka jana, tulivuna hadi tani 20 na chini ya hapo,” anasema.

Hivi sasa hali imeanza kubadilika na baadhi ya wakulima wanaonekana kujawa na hamasa na matumaini ya kufanya vizuri katika kilimo. Hii ni baada ya kufikiwa na mradi endelevu maarufu kama SUSTAIN ambao umejikita zaidi katika kuzalisha mbegu za miwa ambazo baada ya kufanyiwa utafiti na Kituo cha Utafiti wa Miwa Kibaha, imethibitika kwamba zina ubora na uwezo wa kustahamili ukame.

Blackbery yaishtaki Nokia

kwa wizi wa teknolojia

Kampuni ya simu ya Blackberry inaishtaki Nokia kwa madai kwamba kampuni hiyo ya Finland imetumia uvumbuzi wake bila idhini yake.

Madai hayo ya ukiukaji yanahusisha teknolojia inayotumika katika 4G pamoja na mitandao mingine ya simu.

Kampuni hiyo ya Canada inadai kwamba transmita za Nokia pamoja na programu nyingine zinatumia teknolojia yake.

Nokia imeiambia BBC kwamba inalifuatilia swala hilo.

“Tunajua kwamba kuna malalamiko, tutayajadili madai yaliyotolewa na kuchukua hatua zinazohitajika kutetea haki zetu,” alisema msemaji wa kampuni hiyo.

WASICHANA WALIOBOBEA KATIKA TEKNOLOJIA KENYA

Je, unataka programu ya kulipia nauli kwenye gari, ama programu ya kutafuta viungo vya mwili kwenye simu yako?

Wasichana nchini Kenya wanatengeneza programu hizo, chini ya uongozi wa shirika la kimataifa linalowapa wasichana elimu ya kutengeneza programu za simu.

Harriet Karanja, 16, alikuwa kwenye foleni akisubiri kununua tiketi ya kusafiri kwa basi jijini Nairobi, wakati mama mmoja aliyekuwa kwenye foleni alipopokonywa mali yake na wezi.

Aliposimulia tukio hilo kwa wenzake wanne shuleni, aligundua kwamba pia wao walikuwa wameshuhudia tatizo sawa na hilo.

“Itakuwaje iwapo tutabuni njia ya kuwaondoa watu kwenye foleni kununua tiketi?” Harriet akauliza.

Baadaye waliamua kutengeneza programu ya simu (App) ya kurahisisha ununuzi wa tiketi za usafiri, kwa magari ya masafa marefu.

“Programu hii inakuongoza hadi kwenye kituo cha basi kwa kutumia teknolojia ya kugundua maeneo (GPS). Badala ya kwenda kupanga foleni, utaenda tu kusafiri,” anasema Harriet na wameipa jina 'M- Safiri'. BBC

ITAENDELEA WIKI IJAYO

 

Habari Kubwa