Madhara ya kutotambua vipaji-2

02Jan 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
  Madhara ya kutotambua vipaji-2

WIKI iliyopita katika safu hii tuliwaletea sehemu ya kwanza ya mada tajwa hapo juu ambayo kimsingi inazungumzia juu ya umuhimu wa kutambua vipaji mapema, hasa vya watoto na kuvipa fursa ya kukua kwa faida ya mhusika, familia, jamii na taifa kwa ujumla.

Endelea na sehemu ya pili ya mada hiyo kwa leo:

WAZAZI wanapotambua vipaji vyao na kuvifanyia kazi kwa vitendo ni rahisi sana kwa watoto kurithi pia.

Wazazi wanapaswa kuyatendea kazi yale wanayowaambia watoto wao na hii ndio kanuni bora ya malezi.

Hivyo uwezo binafsi wa watoto huchangiwa sana na mazingira ya malezi wanayolelewa kwani watoto hujifunza zaidi kwa kuona vitendo na sio maneno.

Aidha, kama kipaji kinaweza kurithishwa toka kwa mzazi hadi kwa mtoto kutegemea na vinasaba, basi na mazingira ya malezi jinsi yatakavyokuwa kuna uwezekano mkubwa wa mtoto kuwa sawa na wazazi wake.

Kama mzazi atakuwa na kipaji cha uchoraji na mtoto akalelewa katika mazingira ya uchoraji, kuna uwezekano mkubwa wa mtoto kuwa mchoraji pia kutokana na mazingira aliyolelewa, au anaweza kuwa na kipaji cha uchoraji kutokana na vinasaba vya wazazi wake.

Hebu chunguza kwa asilimia kubwa ya watu wenye vipaji, utakuta takribani ukoo mzima una watu wenye uwezo unaofanana.

Chunguza uwezo wa watoto wa walimu utakuta ni mkubwa sana kutokana na malezi waliyolelewa nayo, yaani mazingira ya kitaaluma. Ni nadra sana kukuta mtoto wa mwalimu kuwa na uwezo mdogo wa kitaaluma.

Chunguza familia za waigizaji, waimbaji, n.k utakuta waimbaji hurithisha uimbaji kwa watoto wao kwa njia ya vinasaba na pia kwa njia ya mazingira.

Aidha, chunguza vilevile koo nyingi za viongozi hukuta familia zao ni viongozi wa kada mbalimbali. Vipaji hivi vya uongozi hutokana na mazingira ya malezi waliyolelewa nayo pia kwa njia kurithi vinasaba.

Tunaweza kusema vipaji vinaweza kutengenezwa au kuwezeshwa kutokana na mfumo wa malezi kimazingira yaani kipaji kinaweza kukuzwa kwa njia ya elimu na pia vipaji vinaweza kurithishwa kwa njia ya vinasaba kutoka kizazi hadi kizazi.

Hivyo, tunaweza kurithisha vipaji vyetu kwa watoto wetu kama tutaweza kuwajengea mazingira rafiki kwa kuvifanyia mazoezi vipaji vyetu ili watoto wetu waweze kujifunza kutoka kwetu.

Kama sisi wazazi hatutambua uwezo wetu wa asili wa utendaji kazi ni wazi kabisa tunajenga mazingira magumu kwa vipaji vya watoto wetu.

Watoto wetu wanaweza kutambua vipaji vyao kwa kuwajengea miundombinu mizuri ya elimu, na pia kwa kuanzisha vituo mbalimbali vya maendeleo na ukuzaji wa vipaji.

VIASHIRIA

Viashiria vizuri vya vipaji kwa watoto wetu ndio njia wezeshi ya kuvitambua vipaji. Ili uweze kuvitumia ni lazma tuvitambue kwanza na kisha kuvitumia.

Njia rahisi sana ya mtoto kutambua kipaji chake ni kwa kujaribu vitu vingi sana na kupima uwezo wa utendaji wake katika vitu alivyojaribu kwa kupima kati ya vitu vingi alivyojaribu ni vingapi amefanya vizuri zaidi kuliko vyote?

Kama katika vitu alivyojaribu vipo alivyofanya vizuri kuliko vyote, basi anaweza tambua kipaji chake. Lakini pia njia nyingine ya kutambua kipaji ni kuangalia ni kitu gani mtoto anakipenda kufanya kuliko vyote.

Kile anachokipenda huenda kikawa ndio kipaji chake. Mfano mtoto anapenda sana kuangalia mpira kuliko michezo mingine yote tunaweza sema mtoto huyu anaweza baadaye akawa na kipaji cha uchambuzi wa mpira, akawa mkufunzi (kocha) akawa mwamuzi wa mpira au pia akawa mchezaji mpira mzuri sana.

Aidha, kama mtoto anapenda sana kufuatilia masuala ya muziki mtoto huyu anaweza akawa mwanamuziki mzuri baadaye, mtunzi wa nyimbo au akawa mwalimu wa muziki na pia anaweza akawa mchezaji wa muziki mzuri baadaye.

Kutokana na kutotambua vipaji vyetu na vya watoto wetu tunajikuta katika madhara yafuatayo:

KUTOJITHAMINI

Kipaji au uwezo na nguvu ya asili isipotambuliwa mapema husababisha utendaji kazi hafifu unaotokana na kutojithamini, kwa kujidharau wenyewe katika utendaji kazi katika shughuli mbalimbali za kila siku kwa mtoto.

Kutambua vipaji huanzia utotoni na kadri mtoto anavyoendelea kukua ni vizuri vikatambulika mapema ili kumjengea uwezo wa kujielewa na kuelewa nguvu au uwezo wa asili alionao ili aweze kufanya kazi kwa kujithamini na kuithamini kazi au shughuli anayoifanya ili imletee matokeo mazuri zaidi.

KUTOJIAMINI

Madhara mengine ya kutotambua vipaji ni kutojiamini katika utendaji kazi. Mtoto akijua na kutambua uwezo binafsi alionao atakuwa anajiamini katika kila kitu anachofanya, ila kama hajatambua atakuwa anafanya vitu kwa kubahatisha na kwa wasiwasi mkubwa.

Pia hii huchangia sana kwa mtoto kufanya vitu vingi kwa ufanisi mdogo sana.

Mfano kama uwezo wake upo kwenye mpira wa miguu halafu akakosa fursa ya kushiriki kwenye mchezo huo, akipata nafasi baadaye ya kucheza mpira, hushindwa kujiamini kama anaweza kucheza vizuri kwa sababu ya kutojiamini.

Na sababu ya kutojiamini inatokana na kukosa kwake nafasi ya kujaribu kipaji chake.

Hivyo, mtoto akishajua kipaji chake ni kipi, basi ataweka nguvu kubwa kwenye sehemu hiyo ambayo ana uwezo nayo na uwezo wa kujiamini huwa mkubwa zaidi.

KUCHELEWA KIMAENDELEO

Mtoto asipotambua mapema kipaji au nguvu ya asili na uwezo wa utendaji alionao, atapoteza muda mrefu akifanya mambo mengine asiyoyaweza badala ya kufanya mambo ambayo yapo ndani ya uwezo wake wa kiutendaji.

Na matokeo yake ni kuchelewa kimaendeleo katika masomo, yaani kielimu, na kiuchumi kwa ujumla.

Mfano kama akichelewa na kujitambua ukubwani au akiwa mtu mzima hawezi kuyaona matunda ya kipaji chake zaidi ya kujilaumu akisema ‘laiti ningetambua mapema, ningeshafika mbali kimaendeleo.’

Yaani kwa kifupi, kutotambua kipaji kwa muda muafaka hukwamisha maendeleo ya mtu binafsi na mtoto kwa ujumla.

Yapo madhara mengi yatokanayo na kutotambua vipaji vya watoto wetu, ambayo humuathiri mtoto baadaye akiwa mtu mzima na athari hizi huathiri taifa kwa ujumla siku za usoni.

Maendeleo ya taifa lolote duniani huchangiwa na uwezo binafsi wa utendaji kazi wa wazalishaji.

Ikiwa kama kuna taifa lililoendelea, basi sababu kuu ni uwezo au nguvu ya asili ya kiutendaji wa watu wake ambayo huwa kubwa sana.

Tatizo la mataifa mengi yanayoendelea likiwemo Taifa langu Tanzania kuwa na maendeleo hafifu kunatokana na uwezo mdogo wa utendaji kazi katika uzalishaji, hivyo kushindwa kuzalisha kwa kiwango cha juu, suala ambalo linarudisha maendeleo ya kiuchumi nyuma.

WIKI ijayo nitaelezea namna ya kujitambua kwa wanafunzi.

Mwandishi ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Majengo iliyoko Moshi Tanzania. Anapatikana kwa

Simu: 0674-513851

Facebook page.MwlAndsam

Instragram:Mwl.mwambungu

 

Habari Kubwa