IJUE LESENI YA KUENDESHA GARI BARABARANI- 2

02Jan 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
  IJUE LESENI YA KUENDESHA GARI BARABARANI- 2

WIKI iliyopita katika safu hii tulianza kuelimishana juu ya mada hii ambapo tuliishia katika kipengere cha leseni ya udereva. Tunaendelea kuanzia hapo.

MADARAJA MBALIMBALI YA LESENI

Yapo madaraja 14 katika leseni ya udereva wa vyombo vya moto, ambayo ni pamoja na daraja A, A1, A2 na A3. Daraja A ni kwa ajili ya kuendesha pikipiki zitakazokuwa na ukubwa wa zaidi ya CC 125 au uzito wa kilo 230 ikiwa (isipokuwa pamoja na kigari cha pembeni.

 

Daraja A1ni kwa ajili ya kuendesha pikipiki zenye ukubwa chini ya CC125 au uzito wa kilo 230 na isiyokuwa na kigari cha pembeni. Daraja A2 ni kwa ajili ya kuendesha pikipiki za magurudumu matatu au manne. Daraja A3 ni kwa ajili ya kuendesha pikipiki zisizozidi CC 50.

 

Ukiachana na daraja A, Kuna daraja B, ambalo ni leseni ya kuendesha magari aina zote isipokuwa magari ya biashara, magari ya kubeba abiria (PSV), magari ya kubeba mizigo (HDV) na pikipiki.

 

Kuna vilevile daraja C, C1, C2 na C3. Daraja C ni kwa ajili ya kuendesha magari ya kubeba abiria 30 au zaidi huku C1 ikiwa kwa ajili ya kuendesha magari ya kubeba abiria 15 hadi 29. Kwa upande wa daraja C2, ni leseni ya kuendesha magari ya kubeba abiria 5 hadi 14 na C3 ni maalumu kwa ajili ya abiria wasiozidi wanne.

 

Pia kuna daraja D ambalo ni kwa ajili ya kuendesha magari ya aina zote isipokuwa magari ya abiria, magari makubwa ya mizigo. Kuna daraja E ambalo ni maalumu kwa ajili ya kuendesha magari ya aina zote isipokuwa magari ya abiria (PSV) na pikipiki.

 

Aidha, kuna daraja F ambalo ni maalumu kwa ajili ya kuendesha mitambo ya migodini, ujenzi kama vile Graders, Folklift n.k na kuna daraja G ambalo ni kwa ajili ya kuendesha mitambo ya mashamba kama trekta.

 

Na mwisho kuna daraja H ambayo ni leseni kwa ajili ya kujifunzia kuendesha magari (Learner)

 

UMRI

Mwombaji yeyote wa leseni ya udereva lazima awe na umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea, awe amepita mafunzo, ndipo ataweza kupatiwa leseni kama ifuatavyo;

 

Leseni daraja A, A1, na A2 itatolewa kwa mtu mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea na leseni daraja A3 inatolewa kwa mwombaji mwenye umri wa miaka 16 na kuendelea.

 

Leseni daraja B itatolewa kwa mtu mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea, huku Leseni daraja C itatolewa kwa mwombaji mwenye umri kuanzia miaka 24 mwenye leseni daraja C1 au E yenye kipindi kisichopungua miaka 3 pamoja na cheti cha kufuzu mafunzo ya kuendesha mabasi ya abiria (PSV).

 

Leseni daraja C1 itatolewa kwa mwombaji mwenye umri kuanzia miaka 21 mwenye leseni daraja D yenye kipindi kisichopungua miaka 3 pamoja na cheti cha kufuzu mafunzo ya kuendesha mabasi ya abiria.

 

Leseni daraja C2 na C3 zitatolewa kwa mwombaji mwenye umri miaka 21 ambaye amekuwa na leseni daraja D kwa kipindi kisichopungua miaka 3 pamoja na cheti cha kufuzu mafunzo ya kuendesha magari ya abiria (PSV).

 

Kwa mujibu wa kanuni za SUMATRA za mwaka 2007 (Kif. 17(2) (b) dereva mwenye leseni daraja C, C1 na C2 ataendesha gari la abiria akiwa na umri wa zaidi ya miaka 30 na usiozidi miaka 60.

 

Leseni daraja D itatolewa kwa mwombaji mwenye umri usiopungua miaka 18 na kuendelea, wakati Leseni daraja E itatolewa kwa mwombaji mwenye umri usiopungua miaka 21 ambaye ana Leseni daraja D kwa kipindi kisichopungua miaka 3 pamoja na cheti cha kufuzu mafunzo ya kuendesha magari makubwa ya mizigo.

 

Leseni za daraja F na G zitatolewa kwa waombaji wenye umri wa usiopungua miaka 18 ambao wamepata mafunzo kuhusiana na magari na mitambo husika kwenye chuo chenye sifa kama Kihonda Morogoro.

 

Aidha, Leseni za udereva hutolewa baada ya mtu kuhitimu mafunzo ya udereva.

 

 

Imetolewa na;

Kitengo cha habari, Elimu na mawasiliano,

Makao Makuu ya Jeshi la Polisi.

S.L.P 9141

Dar es Salaam

Baruapepe [email protected], [email protected]

 

ITAENDELEA

 

Habari Kubwa