Z’bar ilivyokwepa kurudia vibatari

20Mar 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Z’bar ilivyokwepa kurudia vibatari

MAZUNGUMZO yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam jana yaliwaokoa wakazi wa Zanzibar kurudi kwenye matumizi ya vibatari, baada ya kukatiwa nishati na Shirika la Umeme (Tanesco), lililokuwa limekusudia.

Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, ilisema Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo amewatoa hofu wakazi wa visiwa hivyo kuwa hawatakatiwa umeme, baada ya Serikali ya Mapinduzi kuanza kulipa deni inalodaiwa.

Kabla ya tamko la Prof. Muhongo, taarifa ya Ikulu ilisema Rais John Magufuli alifanya mazungumzo na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dk. Ali Mohammed Shein.

Mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, taarifa hiyo ilisema zaidi, yalihudhuriwa pamoja na Prof. Muhongo, pia Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Kahitwa Bishaija na Meneja Mwandamizi wa Fedha wa shirika hilo, Sadock Mugendi.

“Prof. Muhongo amesema tayari SMZ imeanza kulipa kiasi cha shilingi bilioni 10 na itaendelea kulipa kidogo kidogo mpaka deni hilo litakapomalizika,” ilisema taarifa ya Ikulu.

Zanzibar ilikuwa katika tishio la kweli la kukatiwa umeme baada ya Tanesco kutangaza Machi 9 kuwa baada ya siku 14 lingesitisha huduma ya umeme kwa wadaiwa sugu wote.

Hadi kufikia Januari, shirika hilo lilikuwa likiwadai wateja wake jumla ya Sh. bilioni 273.4, huku Zanzibar ikilimbikiza karibu nusu ya fedha hizo.

Akiwa ziarani mkoani Mtwara mapema mwezi huu, Rais Magufuli aliagiza Tanesco kuwakatia umeme wateja wote wenye madeni makubwa kwa kampuni hiyo, ikiwamo serikali ya Zanzibar.

Akijibu tishio la Tanesco, Dk. Shein aliwaambia waandishi wa habari Machi 10 kuwa shirika hilo litaikatia umeme Zanzibar kutokana na deni hilo la miaka mingi, watarudi katika matumizi ya vibatari ili kupata mwanga usiku.

Dk. Shein aliyasema hayo mara baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Amaan Abeid Karume, akitokea nchini Indonesia katika mkutano maalumu aliomuwakilisha Rais Magufuli.

Hata hivyo, Dk. Shein alisema pia atashangazwa iwapo umeme utakatwa, ikizingatiwa mahusiano mazuri yaliyopo baina ya pande mbili za muungano wa Tanzania.

HATA IKULU
Akizungumza kabla ya kuweka jiwe la msingi kwenye kituo kipya cha Tanesco mkoani Mtwara, Rais Magufuli alisema tasisi zote za umma zinapaswa kulipa madeni la sivyo zitakatiwa umeme.

"Msiogope, mnapaswa kukata huduma hii kwa taasisi yoyote ambayo hailipi bili zake," alisema Rais Magufuli.

"Nataka kumwambia Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kwamba umeme unapaswa kukatwa hata Ikulu.

"Nikilala gizani, halafu maafisa wa Ikulu ambao hawajalipa watawajibika na sio wewe. Una hakikisho langu kwa hili.

"Pesa za kulipa bili kawaida hutolewa kwa wizara zetu, lakini badala yake hupelekwa kwingine.

"Ninaambiwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haijalipa Sh. bilioni 121. Ninyi (Tanesco) si wanasiasa, mnapaswa kuzingatia majukumu yenu ya kitaaluma... kata huduma ya umeme.

"Nimesema hata kama ni Ikulu, polisi, jeshi ama shule... hakuna mwenye deni anayepaswa kuachwa. Ni kwa njia hii tu tunaweza kuhakikisha kwamba pesa zilizotengewa wizara kwa ajili ya umeme zinatumiwa kama ilivyopangwa ili Tanesco iweze kuendesha kazi zake na kushughulikia matatizo ya uhaba wa umeme.

"Tanesco haiwezi kuboresha huduma kwa sababu ya madeni ya serikali yasiyolipwa."

Habari Kubwa