Wigo bima ya afya wapanuliwa kunufaisha wengi

21Apr 2017
Beatrice Shayo
Nipashe
Wigo bima ya afya wapanuliwa kunufaisha wengi

SERIKALI imepanua wigo wa bima ya afya kwa kushirikisha sekta binafsi ili kupunguza pengo lililopo kutokana na asilimia 27 ya Watanzania kwa sasa ndio wanaonufaika na huduma hiyo.

bima ya afya.

Katika kutekeleza azma hiyo, jana ilizinduliwa huduma nyingine ya bima ya afya ijulikanayo kama Afya Wote, ambayo imebuniwa na kampuni ya bima ya Zurich Insurance Brokers kwa kushirikiana na Jubilee Tanzania.

Akizunguimza wakati wa uzinduzi wa bima hiyo mpya jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Edward Mbanga, alisema nia ya serikali ni kuhakikisha Watanzania wote wanapata bima ya afya ili kupunguza mzigo wa gharama za matibabu.

Alisema baada ya sera kubadilika na wananchi kutakiwa kuchangia huduma za afya, serikali bado inasisitiza wananchi kutakiwa kujiunga katika bima za afya ambazo zinatolewa na taasisi za serikali na za binafsi.

Akizungumza hali ya sasa, Mbanga alisema asilimia 27 ya Watanzania ambao ni takriban milioni 14 kati ya milioni 50 ndio wako katika mfumo wa bima ya afya. Kwa mantiki hiyo, alisema takriban Watanzania milioni 36 wanalazimika kuingia mifukoni kugharimia huduma za matibabu.

‘Hii bado ni changamoto kubwa katika huduma za afya ikizingatiwa kuwa idadi kuwa ya Watanzania ni wa kipato cha chini na wakati huo huo gharama za matibabu ni kubwa, hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuhamasisha wananchi wengi kujiunga na bima ya afya,” alisema.

Mbanga alisema kuanzishwa kwa Afya Wote kutasaidia kupunguza pengo hilo na kupongeza Jubilee na Zurich kwa kubuni mpango huo ambao utasaidia wananchi wengi kupata huduma za matibabu kwa gharama nafuu.

“Utafiti kamili wa wanaokosa matibabu bado hatuna lakini kama taifa tuna sera ya msamaha kwa sababu Mtanzania hawezi kufa kwa sababu hana fedha. Lakini hii haitupi hali nzuri ya wananchi kufikia huduma ya afya kwa uhakika zaidi kutokana na kukosa bima ya afya,” alisema Mbanga.

Naye Mkuu wa Idara ya Afya wa Jubilee, Kenneth Agunda, alisema matibabu kwa wanachama wa Afya Wote yatatolewa katika zaidi ya hospitali 200 za umma na binafsi ambazo zinatumia bima ya Jubilee.

Kuhusu gharama, Agunda alisema mwanachama atachangia Sh. 174,000 kwa mwaka na atapata huduma za afya na wategemezi watatu.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya bima ya Zurich Sudi Simba, kwa upande wake alisema wameungana na ya Jubilee kuanzisha bima hiyo ya afya ili kuwawezesha Watanzania kupatiwa matibabu yenye uhakika na kwa gharama nafuu.

“Sisi ndio tuliobuni wazo hili na Jubilee kukubali baada ya kuona kumekuwa na matatizo katika kupata huduma za afya na lengo letu ni kusaidia harakati za serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kwa bei nafuu,” alisema Simba.

Habari Kubwa