Waziri Mabula ageuka mbogo madeni ya ardhi

19Mar 2017
Cynthia Mwilolezi
Nipashe Jumapili
Waziri Mabula ageuka mbogo madeni ya ardhi

NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo na Makazi, Angelina Mabula amekuwa mbogo dhidi ya watumishi wa halmashauri za Mkoa wa Arusha,

NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo na Makazi, Angelina Mabula.

Baada ya kubaini ukwepaji wa uingizaji taarifa za viwanja na mashamba kwenye mfumo wa kielekroniki na kusababishia serikali kukosa kodi ya zaidi ya Sh. bilioni 170.

Akizumgumza jana huku akilazimika kukagua mifumo ya kielekroniki ya halmashauri ya Jiji la Arusha, Meru na Wilaya ya Arusha na Arumeru, wakati wa ziara ya kikazi jana, Mabula alisema inasikitisha kuona watumishi hao wanakwepa kuingiza taarifa za viwanja na mashamba waliyo nayo katika mfumo elekezi wa serikali na kubaki katika mfumo wa zamani wa mafaili.

Alisema hali hiyo inafanywa kwa makusudi ili kujinufaisha au kwa sababu wanazofahamu, hali ambayo serikali haiwezi kukubaliana nayo zaidi ya kuwaondoa watumishi watakaobaki katika hali hiyo.

“Sasa natoa mwisho Juni 30, mwaka huu, muwe mmeshaweka viwanja na mashamba yote mliyonayo katika mfumo huu, ili wizarani iwe rahisi kufuatilia nani amelipa kodi kuliko ilivyo sasa. Taarifa haziingizwi katika mfumo na zile chache zilizoingizwa zimejaa madudu ambapo unakuta kiwanja kina namba lakini hakina jina la eneo kilipo au kipo eneo fulani hakuna namba,” alisema.

Alisema endapo mtu atashindwa kutimiza hilo, ajue wapi atakwenda kwa sababu serikali haiwezi kuvumilia kukaa na watumishi wasiojituma, kwa kuwa mfumo huo tangu uanze una zaidi ya miaka miwili sasa, lakini watumishi wa ardhi wanasuasua kuingiza taarifa kwa sababu ya kupiga ‘dili’.

Kutokana na hali hiyo, mabula alisema watumishi hao wamesababisha hasara ya mabilioni ya shilingi kwa serikali.

Alitaja kila halmashauri na viwango vya hasara kwenye mabano kuwa ni Jiji la Arusha (Sh. bilioni 68), Arusha DC (Sh. bilioni 49), Karatu (Sh. bilioni 27), Meru (Sh. bilioni sita), Longido (Sh. bilioni 15), Monduli (Sh. bilioni tano) na Ngorongoro Sh. bilioni 3.

“Endapo mtaingiza taarifa zenu, hizi fedha zitapatikana na tutapata zaidi ya hizi. Wale wasiolipa watafuatiliwa kwa wakati tofauti na sasa Kiswahili kinakuwa kingi, mara mtu ana hati lakini halmashauri haiwezi kumfuatilia alipe kodi kwa madai hawafahamu alipo, kitu ambacho hakiwezekani ni ubabaishaji wa dili,” alisema.

Aidha aliagiza halmashauri zote nchini kupeleka notisi ya siku 14 kwa wadaiwa sugu na atakayeshindwa kulipa afilisiwe ili fedha ziingizwe serikalini.

Pia alisema kuna umuhimu wa kuelimisha wananchi kuwa gharama za hati miliki za viwanja na shamba kuwa imepunguzwa toka asilimia 15 hadi asilimia 2.5, hivyo hakuna sababu ya kushindwa kuwa na hati miliki ili watambulike kisheria.

Akizungumza baada ya maagizo hayo kutolewa, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Athumani Kihamia, alisema fedha ambazo anadaiwa ni za tangu mwaka 1984 ilipoanzishwa halmashauri hiyo hadi sasa.

Habari Kubwa