Wazee Z’bar wadai ‘matapeli’ kuchukua pensheni zao

16Apr 2017
Rahma Suleiman
Nipashe Jumapili
Wazee Z’bar wadai ‘matapeli’ kuchukua pensheni zao

JUMUIYA ya Wazee Zanzibar imesema inasikitishwa na tabia ya baadhi ya watu ambao sio waaminifu wanaopokea fedha ya pensheni inatolewa na Serikali ya Zanzibar kwa wazee wote waliofikia umri wa miaka 70 kila mwezi.

RAIS WA ZANZIBAR DK ALI MOHAMED SHEIN

Akizungumza na waandishi wa habari, mwanzilishi wa jumuiya hiyo, Hashim Bakari, alisema baadhi ya watu huenda kupokea pensheni hizo kwa niaba zao na kutowafikishia zote.

Alisema katika jumuiya yao wameshapokea malalamiko mengi kutoka kwa wazee kuwa fedha ya pensheni zinazotolewa na serikali kila mwezi Sh. 20,000, huambulia Sh.10,000 na wengine hawapati kabisa.

“Wapo baadhi ya wazee ambao hawajiwezi, huwatuma watoto wao au watu wanaowaamini kwenda kuwachukulia fedha hizo, lakini baadhi yao huwa sio waaminifu na badala yake hujichukulia mamlaka kuzichukua na kumkosesha mzee haki yake,” alisema.
Alisema kuna wazee 400 hawakupata pensheni zao katika mwezi uliopita.

“Wapo baadhi ya wazee leo wapo Magomeni, kesho utasikia kachukuliwa na mtoto wake yupo Makunduchi, hivyo inakuwa vigumu kupewa fedha hizo wakati akiwa Makunduchi na yeye ameandikishwa Magomeni,” alisema.

Katibu wa Jumuiya hiyo, Amani Suleiman Kombo, alisema ni mwaka mmoja tangu serikali ianze kutoa fedha hizo kila mwezi kwa wazee waliofikia umri wa miaka 70, ili iweze kuwasaidia katika kujikimu kimaisha.

“Tunampongeza Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein kwa kutupatia kiwango cha elfu ishiri kila mwezi kwa wazee wote waliofikia umri wa miaka 70 na tokea ilipoanza kutolewa Aprili mwaka jana, hakuna hata mwezi mmoja tulioambiwa kuwa serikali haina fedha,” alisema.

Alisema licha ya Zanzibar kuwa na uchumi mdogo, kulinganisha na nchi zengine zilizoendelea, lakini inajitahidi kuwapatia wazee fedha hiyo.

Alisema kwa mwaka 2016 wazee 21,750 waliofikia umri wa miaka 70, walisajiliwa kwa ajili ya kupatiwa fedha hiyo na mwaka huu ongezeko la wazee waliofikia umri huo limeongezeka na kufikia 26,484.

Alisema, vituo 36 Unguja vimefunguliwa katika utoaji wa huduma hiyo ya fedha za pensheni kwa wazee na wengi wao wamekuwa wakijitokeza au kuwawakilisha watoto wao kuwachukulia.
Aliwasihi waliaminiwa kuwawakilisha wazee wao kuhakikisha wanawafikishia fedha hizo.

Habari Kubwa