Watano wafa mapambano na polisi

03Nov 2017
George Tarimo
Nipashe
Watano wafa mapambano na polisi

JESHI la Polisi mkoani Iringa limewaua watu watano wanaotuhumiwa kuwa majambazi katika eneo la Ruaha Mbuyuni wilayani Kilolo katika majibizano ya risasi na polisi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Julius Mjengi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Julius Mjengi, alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana majira ya saa 22:45 usiku katika eneo la Kware, Ruaha Mbuyuni.

Alisema watu hao walionekana kwenye eneo hilo wakiwa na lengo la kuwapora baadhi ya wafanyabiashara wa eneo hilo ndipo polisi walipopata taarifa na kwenda kwenye eneo la tukio.

“Jeshi la Polisi lilipata taarifa kutoka kwa wasamaria wema wa eneo hilo na kuanza msako mkali. Ilipofika 22:45 majambazi hao walionekana wakiwa wamejificha kwenye kichaka karibu na korongo lililopo kwenye eneo hilo,” alisema.

Kamanda Mjengi alisema watu wawili kati ya hao walifariki dunia papo hapo na watatu walijeruhiwa vibaya, lakini baadaye walifariki dunia wakati wanapelekwa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Iringa.

Mjengi alisema watu hao bado hawajafahamika kwa majina yao huku akisema jumla yao walikuwa sita, lakini mmoja alitoroka na kwamba msako wak umtafuta bado unaendelea.

Alisema katika mashambulizi hayo, zilikamatwa silaha mbili, ambazo ni bunduki aina ya SMG na risasi 26 zikiwa kwenye magazine na bastola aina ya Star ikiwa na risasi sita kwenye magazine. Alisema silaha zote zilifutwa namba za usajili.

Habari Kubwa