Watakiwa kujiimarisha kilimo cha korosho

21Mar 2017
Nathan Mtega
Nipashe
Watakiwa kujiimarisha kilimo cha korosho

WAKAZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, wametakiwa kujiimarisha zaidi katika kilimo cha zao la korosho.

Aidha, wametakiwa kuhakikisha kwamba wanazalisha zao hilo katika ubora unaoweza kushindana na soko la ndani na nje ya nchi.

Akizungumza kuhusu uzalishaji bora wa korosho na mazao mengine, Munge wa Tunduru Kusini, Daimu Mpakate, alisema zao hilo kwa sasa lina soko kubwa na lenye ushindani mkubwa.

Mpakate alisema kwa kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani, wakulima wanapata fursa ya kukutana moja kwa moja na wanunuzi ambao wamekuwa wakijitokeza kwenye mnada na kushindana kwa bei, lakini wanunuzi wataendelea kufanya hivyo ikiwa korosho zinazozalishwa wilayani humu zitakuwa na ubora unaotakiwa sokoni na kwa walaji.

Alisema upo uwezekano wa bei ya korosho kuongezeka msimu hadi msimu ikiwa ubora wa korosho utaongezeka kwa wakulima kujitahidi kuzingatia njia bora za uzalishaji wa zao hilo.

Mbunge huyo alisema msimu wa mwaka jana korosho ziliuzwa kwa Sh. 3,800 kwa kilo moja na wanunuzi walifikia hatua ya kugombania soko kwa sababu ya ubora wa korosho pamoja na wakulima kuukubali mfumo wa stakabadhi ghalani ambao umepangwa kuboreshwa zaidi kwa kushirikiana na wakulima wenyewe na wadau wengine.

Nao baadhi ya wakulima pamoja na kupongeza mpango huo wa stakabadhi ghalani kwa kukiri kuwanufaisha kwa kiasi kikubwa, wameiomba serikali kuhakikisha pembejeo zinawafikia kwa wakati ili waende sambamba na msimu wa uzalishaji wa zao hilo pamoja na mazao mengine yatakayowaezesha kujikwamua zaidi kiuchumi.

Mazao hayo ni pamoja na mbaazi, mpunga na ufuta na wakulima hao walisisitiza kuimarishwa pia kwa soko la mazao hayo kama inavyofanyika kwenye zao la korosho.

Aidha, Mbunge Mpakate amewahakikishia wananchi na wakulima kuwa atashirikiana na serikali kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili katika uzalishaji wa mazao mbalimbali wanayoyategemea kujikwamua kiuchumi.

Pia aliwataka kuhakikisha wanawapeleka watoto shuleni na kufuatilia maendeleo yao badala ya kuwaachia walimu pekee yao kwani ni jukumu la kila mzazi kufuatilia maendeleo ya mwanawe kwa kushirikiana na walimu.

Habari Kubwa