Wastaafu wa PSSSF sasa wasotea pensheni miezi 4

23May 2019
Salome Kitomari
DAR
Nipashe
Wastaafu wa PSSSF sasa wasotea pensheni miezi 4

WASTAAFU wa Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), wameendelea kusotea pensheni yao ya kila mwezi kwa miezi minne sasa.

 

Wastaafu hao waliozungumza na Nipashe, Aprili mwaka huu, baada ya kugoma kuondoka kwenye ofisi ya PSSSF mkoa wa Ilala, walisema hawajalipwa tangu Februari mwaka huu.

 

 

Wakizungumza jana na Nipashe kwa nyakati tofauti, wastaafu hao walisema majibu wanayoendelea kupewa ni kuwa majina yao hayajaingizwa kwenye mfumo yalisahaulika.

 

“Hadi sasa hatujalipwa na hatujui lini hasa wataanza kutulipa, wamesema wanaingiza majina yetu kwenye mfumo. Tunapata shida, tunaomba serikali itusaidie katika hili,” alisema mmoja wa wastaafu.

 

Aidha, wastaafu hao ambao wametofautiana miezi ya kudai pensheni ya kila mwezi, walisema waliwasilisha taarifa zao muhimu, lakini bado tatizo la kutoonekana kwenye mfumo limeendelea kuwapo, hivyo kuwafanya waishi maisha magumu kwa kuwa fedha hizo wanazitegemea kwa mahitaji yao ya kila siku.

 

“Sijalipwa pensheni yangu ya mwezi kwa miezi minne sasa, ila naamini serikali itatulipa, lakini ni vyema kukawa na mawasiliano juu ya lini hasa watamaliza kuweka majina yetu kwenye mfumo na kuanza kutulipa,” alisema mstaafu kutoka mkoani Kilimanjaro.

 

Wastaafu hao walisema licha ya kuchanga kwa uaminifu kwa kipindi chote walichokuwa wanafanyakazi, lakini imefika wakati wa kulipwa fedha zao kila mwezi wamejikuta katika wakati mgumu.

 

Mmoja wa wastaafu aliyestaafu 2012, alisema alihakiki taarifa zake Februari mwaka huu, lakini hadi sasa anaelezwa tatizo ni uhakiki wa taarifa, na kwamba zimekusanywa na kutumwa Dodoma.

 

Mwingine alistaafu mwaka 2011, na alishahakiki taarifa zake na alikuwa akipata pensheni ya kila mwezi, lakini kwa sasa hapati na kwamba ndiyo fedha aliyokuwa anaitegemea kwa ajili ya kuendeshea maisha yake.

 

Mwingine alistaafu mwaka 2017 na kwa miezi minne sasa hajalipwa pensheni ya mwezi, kwa sababu ya kuelezwa kuwa majina yao hayajaingizwa kwenye mfumo.

 

Meneja wa PSSSF mkoa wa Ilala, James Mlowe, alipozungumza na wastaafu hao mwezi uliopita, alithibitisha kuwapo kwa tatizo hilo kutokana na mfumo mpya baada ya mifuko kuunganishwa, na kwamba katika kuingiza majina ya wastaafu wapo waliosahaulika licha ya kufanya uhakiki.

 

“Tunafanya tuwezalo kuwa kabla ya Mei 25, mwaka huu, wawe wamelipwa fedha zao zote za nyuma, hili ni tatizo la kimfumo lilijitokeza ila linashughulikiwa baada ya uhakiki wa wastaafu kuanzia Januari hadi Machi, mwaka huu, ambao hawajahakikiwa walitolewa kwenye daftari, wapo waliohakikiwa, lakini mfumo haukuwatambua kutokana na uchanga wa mfumo husika,” alisema.

 

Alisema PSSSF ina wastaafu 124,000, na kwamba kitakachofanyika ni kuandaa malipo kwa ajili ya wachache ambao majina yao yalirukwa wakati wa kuingiza taarifa kwenye mfumo.

Habari Kubwa