Wasoma chini ya mti kwa kukosa vyumba vya madarasa

14May 2017
Robert Temaliwa
Nipashe Jumapili
Wasoma chini ya mti kwa kukosa vyumba vya madarasa

MKOA wa Pwani, Idara ya Elimu unakabiliwa na uhaba wa vyumba vya madarasa 3,973 hali  inayosababisha baadhi ya wanafunzi kusomea chini ya miti.

Hayo yalisemwa juzi na Ofisa Elimu Mkoa wa Pwani, Germana Sendoka, katika maadhimisho ya kilele cha wiki ya elimu, wakati alipokuwa akitoa taarifa ya hali ya kitaaluma na changamoto zinazoikabili idara hiyo ambayo yalifanyikia wilayani hapo.

Sendoka alisema kutokana na uhaba huo, wanafunzi wanarundikana hadi kufikia 200 katika darasa moja huku wengine wakilazimika kusomea chini ya miti.
Alisema mkoa huo una jumla ya vyumba vya madarasa 3,003 huku mahitaji yakiwa ni  6,976.

Kwa upande wa nyumba za walimu, alisema mkoa huo una nyumba 1,798 huku mahitaji yakiwa 6,609 na upungufu ni 4,811.

Sendoka alisema upungufu wa nyumba za walimu pia unasababisha kupunguza morali ya kufundisha kwa walimu hasa shule za maeneo ya vijijini ambako hakuna nyumba za kupanga.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo, alisema pamoja na juhudi zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuongeza miundombinu ya shule, miundombinu hiyo haitoshi.

Ndikilo alisema wanahitaji mkoa na halmashauri zake zote, wazazi, walezi na wadau ujipange kupunguza ama kuondoa changamoto hizo kila moja katika eneo lake.

Aliongeza kwa kukemea uwepo wa tafsiri potofu ya dhana ya elimu bila malipo kwa kuwa ni miongoni mwa mambo yanayorudisha nyuma ufanisi wa kiutendaji katika sekta ya elimu.

Alisema kutokana na tafsiri hiyo, wazazi na wanajamii wengi wanaona hawana wajibu wa kuboresha mazingira ya utoaji wa elimu mashuleni wakiamini ni jukumu la serikali pekee jambo ambalo si la kweli.

“Waraka wa elimu bila malipo namba 6 wa mwaka 2015, kuhusu utekelezaji wa elimu bila malipo umebainisha wazi majukumu ya kila mdau wa elimu wakiwamo wazazi, walimu, bodi za shule na jamii kwa ujumla namna ya kushiriki kutekeleza hilo,” alisema Ndikilo.

 

Habari Kubwa