Wanawake wanaodaiwa kuvishana pete wazidi kusota

14Dec 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Wanawake wanaodaiwa kuvishana pete wazidi kusota

HATIMAYE Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limewafikisha mahakamani watuhumiwa wanawake wawili wanaotuhumiwa kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja, Milembe Suleiman na Janeth Shonza pamoja na wenzao wawili wakikabiliwa na mashtaka matatu, huku hatima ya dhamana yao ikijulikana kesho. 

Wanne hao walifikishwa mahakamani jana mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza na kusomewa mashtaka matatu ya makosa ya kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja  na makosa ya kimtandao.

Akisoma mashtaka hayo mahakamani jana mbele ya Hakimu Mwandamizi Greyson Sumaye kwa niaba ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Wilbert Chuma, Wakili wa Serikali, Emmanuel Luvinga, aliieleza mahakama kuwa watuhumiwa hao wanakabiliwa na makosa matatu tofauti.

Wakili Luvinga alidai kuwa shtaka la kwanza ni kufanya vitendo vinavyoashiria mapenzi ya jinsia moja linalowahusu Milembe na Janeth.

Wakili huyo alidai kuwa shtaka la pili wanalokabiliwa nalo ni kusambaza video yenye vitendo vinavyoashiria mapenzi ya jinsia moja linalowahusu wawili hao pia.

Katika shtaka la tatu linalowahusu Aneth Mkuki na Richard Fabian, Wakili Luvinga alidai kuwa wawili hao wanashtakiwa kwa kosa la kuandaa sherehe kwa ajili ya Milembe na Janeth kuvishana pete ya uchumba.

Kutokana na mashtaka hayo, Mahakama ilieleza kuwa itatoa uamuzi wa hoja dhidi ya washtakiwa katika kesi hiyo kesho kama wanastahili dhamana au la.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha hati mahakamani hapo ukiomba mahakama hiyo kutowapa dhamana kwa sababu mbalimbali huku upande wa utetezi ukidai ni haki ya washtakiwa kupewa dhamana.

Katika shauri hilo namba 548/2017, Wakili Luvinga alidai katika hati hiyo kuwa RCO (Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa)  anaomba washtakiwa hao wasipewe dhamana kwa kuwa upelelezi bado haujakamilika na kwamba kitendo hicho ni kinyume cha maadili ya Kitanzania.

Wakiwasilisha hati pinzani, Wakili wa upande wa utetezi, Mashaka Tuguta akisaidiana na Augustine Kulwa na Jebra Kambole, waliiomba mahakama kuwapa dhamana washtakiwa kwa kuwa ni haki yao kisheria.

Hakimu Chuma alisema atatoa uamuzi wa hoja kesho, hivyo washtakiwa kurudishwa rumande.Novemba 30, mwaka huu, Milembe ambaye ni Ofisa wa Mgodi wa Geita anayehusika katika kitengo cha ununuzi, alikamatwa na Jeshi la Polisi alidaiwa kujihusisha na vitendo vya mapenzi ya jinsia moja.

Mwanamke huyo alikamatwa ikiwa ni siku chache baada ya kusambaa kwenye mitandao ya kijamii kwa video inayodaiwa ni ya mwanamke huyo akionekana akimvisha pete ya uchumba mwanamke mwenzake anayedaiwa ni Janeth.

Habari Kubwa