Wakuu wa Mkoa, Wilaya waonywa

17Jul 2017
Frank Monyo
Nipashe
Wakuu wa Mkoa, Wilaya waonywa

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) umewataka wakuu wa Mikoa na Wilaya kuacha kutumia vibaya madaraka yao kwa kukamata watu hovyo kwani kwa kufanya hivyo ni kuminya uhuru na haki za binadamu.

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam jana na Mratibu THRDC, Onesmo Olengurumwa, wakati wa kutoa tamko la kulaani kukamatwa kwa watetezi wawili wa haki za binadamu katika wilaya ya Kishapu Mkoa wa Shinyanga wakiwa katika majukumu yao.

Alisema kuwa tangu mwanzoni mwa mwaka huu mpaka sasa kuna matukio zaidi ya 20 ambayo yameripotiwa ya kukamatwa na kuzuiwa kufanya kazi watetezi wa haki za binadamu wakiwa katika majukumu yao.

Alisema hivi sasa Taifa linapitia kipindi kigumu kwa vitendo vya kuminywa kwa haki za binadamu, kutokana na matamko na amri za wakuu wa mikoa na wilaya kuwaweka watu mahabusu kwa kutumia madaraka yao huku wakivunja haki za binadamu.

Olengurumwa aliwataja waaliokamatwa wilayani Kishapu 12 Julai mwaka huu kuwa ni Bibiana Mushi na Nicodemus Ngelela ambao wanatoka katika shirika la Actions for Democracy and Local Governance ADLG ambalo linapigania ushiriki wa wananchi, demokrasia na utawala bora katika Mkoa wa Shinyanga.

"Ongezeko la kuminywa kwa nafasi ya Asasi za Kiraia / Watetezi Nchini zimekuwa zikiongezeka kwa tabia ya wakuu wa Mikoa na Wilaya kutumia nguvu pasipo busara kupitia nguvu walizopewa," alisema Olengurumwa.

Habari Kubwa