Wakongo, Warundi vinara wageni ‘wanaojilipua’ Dar

28Dec 2017
Ibrahim Joseph
Nipashe
Wakongo, Warundi vinara wageni ‘wanaojilipua’ Dar

RAIA kutoka nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Burundi na Rwanda ndiyo wanaoongoza ‘kujilipua’ kwa kuingia nchini kinyume cha sheria na kukutwa katika maeneo mbalimbali ikiwamo jijini Dar es Salaam.

Msemaji wa Jeshi la Uhamiaji, Mrakibu Ally Mtanda.

Mbali na jiji la Dar es Salaam linaloshika nafasi ya tatu kwa kukutwa na raia wengi wa kigeni waishio kinyume cha sheria, mikoa mingine ni Kigoma inayoongoza na Kagera. Ijapokuwa ‘kujilipua’ siyo neno rasmi, lakini baadhi ya watu hasa kwenye jiji la Dar es Salaam hulitumia kuelezea wageni wanaoishi katika nchi nyingine kinyume cha utaratibu.

Taarifa iliyotolewa jana na Msemaji wa Jeshi la Uhamiaji, Mrakibu Ally Mtanda, ni kwamba kwa ujumla, kuna wahamiaji haramu 7,033 waliokamatwa nchini katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Septemba mwaka huu, mkoa wa Kigoma uliongoza kwa kuwa na wahamiaji hao 388. Mingine ni Kagera iliyokutwa na wahamiaji haramu 347, Dar es Salaam (198), Tabora (163), Mara (85), Shinyanga (84), Njombe (31) na Morogoro (28). Wengine walikamatwa katika maeneo mengine mbalimbali nchini.

“Mkoa wa Kigoma unaongoza kwa kuingiza wahamiaji haramu wengi kuliko mikoa yote kutokana na kupakana na nchi zenye vurugu za kivita,” alisema Mtanda.

Msemaji huyo aliongeza kuwa wengi wa wahamiaji hao haramu hutoka katika nchi jirani za Kongo, Burundi na Rwanda kutokana na hali ya usalama kuwa ndogo katika nchi zao.

Aidha, alisema katika kipindi hicho, wageni waliokamatwa wakiingia nchini kinyume cha utaratibu kutoka katika nchi za Ethiopia na Somalia walikuwa 858 na wengi wao huwa na kawaida ya kuingia nchini kwa kupitia njia za panya kwenye mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Tanga, wakiwa safarini kwenda kutafuta maisha nchini Afrika Kusini.

Mtanda aliyataja baadhi ya maeneo ambayo wahamiaji hao haramu hukamatwa kutokana na operesheni mbalimbali za kuwasaka huwa ni kwenye vituo vya mabasi, barabarani, kwenye vyombo vya usafiri, nyumba za kulala wageni, viwandani na pia mashambani. Wahamiaji hao haramu hufikishwa mahakamani na kuadhibiwa kwa kufungwa, kulipishwa faini na wengine kurudishwa kwenye nchi zao. 

Habari Kubwa