Waiomba serikali kuwajengea kivuko 

31Dec 2017
Neema Emmanuel
Nipashe Jumapili
Waiomba serikali kuwajengea kivuko 

WANANCHI wa Kisiwa cha Kome kilichomo ndani ya Ziwa Victoria wilayani Sengerema mkoani Mwanza, wameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuongeza kivuko kingine ili kuondoa kero ya usafiri na msongamano wa abiria na magari iliyodumu kisiwani humo kwa muda mrefu.

Kisiwa cha Kome kilichomo ndani ya Ziwa Victoria

Wanasema shida hiyo huwasumbua kila wakati wananchi hao wanapohitaji kuvuka ng’ambo kwenda  maeneo mengine ya kisiwa hicho kwa shughuli za uchumi na kijamii.

Waliyabainisha hayo wakati walipotembelewa na Naibu Waziri wa Ujenzi , Uchukuzi na Mawasiliamo, Elias Kwandikwa, akiwa  eneo la Nyakalilo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa, kukagua miundombinu ya barabara pamoja na vivuko.

Michael Boniphace, mkazi wa Kome na Yusta Joseph wa Nyakalilo ni baadhi ya wananchi walioelezea changamoto hiyo na kusema kuwa kufuatia kivuko kilichopo hivi sasa cha MV Kome, kuanza kuelemewa na wingi wa abiria pamoja na mizigo, kama magari ya  samaki hali inayotishia usalama majini.

Aidha, Naibu Waziri Kwandikwa, baada ya kushuhudia adha ya usafiri wanayokutana nayo abiria wa kivuko cha MV Nyakalilo, kinachofanya safari zake kuelekea kisiwa cha Kome,aliahidi kushughulikia changamoto hiyo ili wakazi wa visiwa hivyo waweze kupata usafiri wa uhakika.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Buchosa ambaye pia ni Waziri wa Kilimo Dk. Charles Tizeba, alisema kivuko hicho kinachobeba abiria zaidi 100 na kufanya safari tano kwa siku, hivi sasa kimeanza kuzidiwa na wingi wa abiria, hali inayosababisha kuwapo kwa usumbufu mkubwa wa usafiri huo.

Hata hivyo, aliwapa matumaini kuwa maombi yao yamefikishwa katika idara husika ili changamoto hiyo itatuliwe.

Habari Kubwa