Waiomba serikali kufuta vibali vya waganga wa jadi

01Jan 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Waiomba serikali kufuta vibali vya waganga wa jadi

UMOJA wa madhehebu ya dini mkoani Geita, umeiomba serikali kufuta vibali vya waganga wa tiba asilia na tiba mbadala ili kudhibiti matukio ya mauaji ya walinzi na wanawake wazee yanayoendelea mkoani hapa.

Ombi hilo limetolewa jana na Padri Paulo Mwalongo, kutoka Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), wakati wa ibada maalumu ya kuliombea amani taifa la Tanzania.

Alisema waganga wa tiba asilia na tiba mbadala waliopewa vibali vya muda na serikali, baadhi yao wanavitumia vibaya hivyo kuiomba serikali kufuta vibali vyote na kuanza mchakato wa kutoa vibali hivyo upya baada ya kuwachunguza.

Alisema matukio ya kuawa kwa walinzi kikatili, wanawake vikongwe na watu wenye ulemavu wa ngozi kunyofolewa viungo vyao yana husishwa na imani za kishirikina na chanzo chake ni waganga kupiga ramli chonganishi.

Alitaka hatua za haraka zichukuliwe kukomesha hali ya matukio hayo ambayo yamekuwa yakitokea kila kukicha.

“Serikali ichukue hatua madhubuti kwa kufuta vibali vya waganga hao vinawapa viburi na baadhi wanavitumia vibaya mchakato wa kuwapa uanze upya baada ya kuwasajili na kuwahakiki kama wameacha kupiga ramli chonganishi,” alisema.

Askofu Josephat Saguda kutoka (CPCT), alisema wanaoua binadamu wenzao na kumwaga damu, wanaleta laana katika taifa na hivyo kuwataka wote wanao jihusisha na matukio hayo kujisalimisha wenyewe kwa mwenyezi Mungu.

Kaimu Sheikh Bashiru Haruna wa Mkoa wa Geita (Bakwata), alisema amani na upendo vikitoweka nchini, hakuna serikali tena na hivyo kuitaka kukomesha hali ya matukio hayo yanayo ashiria amani kutoweka.

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mwalimu Hermani Kapufi, alisema serikali wilayani Geita ina kusudia kufuta vibali vyote vya waganga hao ifikapo Januari 30, 2017 kudhibiti matukio ya walinzi, vikongwe na albino.

Aliwataka viongozi wa dini kuendelea kuliombea taifa amani na kudumisha upendo kwa kuwa dini ni daraja linalo sababisha watakatifu kufika mbinguni.

Habari Kubwa