Vijana kufunzwa uzalendo , utaifa

26Nov 2017
Joseph Mwendapole
Nipashe Jumapili
Vijana kufunzwa uzalendo , utaifa

RAIS John Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa kampeni kubwa ya kitaifa ya uzalendo na utaifa itakayofanyika mwezi ujao mkoani Dodoma.

Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, wakati akizungumza kwenye mkutano na wadau mbalimbali kuhusu kampeni hiyo.

Wizara ya Habari iliitisha mkutano na wadau mbalimbali ili kujadili namna ya kuwezesha kampeni hiyo kufanikiwa ikiwamo namna ya kupata Sh. milioni 350 zinazohitajika kufanikisha kampeni hiyo.

Dk. Mwakyembe alisema kampeni hiyo ni muhimu ili kuwaelimisha vijana kujua Tanzania ilikotoka na namna babu zao walivyopata shida kupambana na ukoloni hadi wakapata uhuru.

“Vijana wengi walizaliwa baada ya uhuru na wengi wao kwa sasa ndio wanashika hatamu za uongozi, hawajui shida ambayo babu zao alipata kupambana na wakoloni sasa sisi ambao tulikuwepo lazima tutende haki kwa kuwapa hiyo historia,” alisema Waziri Mwakyembe.

Alisema hivi sasa kuna tatizo kubwa la mmomonyoko wa maadili na kushamiri kwa vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa mali za umma, chanzo ikiwa ni watu kukosa uzalendo wa kuipenda nchi yao.

Aidha, alisema Wizara yake imeliona tatizo hilo na kwa kuwa hakuna wa kumlaumu imeona ni wakati mwafaka wa kuziba pengo hilo kwa kuanzisha kampeni ya kitaifa ya uzalendo na utaifa.

“Nilipoenda Ujerumani kusomea PhD nilikuta wanatoa ufadhili wa fedha nyingi sana kwa wanafunzi wanaosomea historia nikamuuliza Profesa wangu kwanini, akasema kama huwezi kujua uliokotoka basi huwezi kuwa na uhakika na kule unakotaka kwenda,” alisema

Dk. Mwakyembe alimpongeza MKurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Pensheni wa PSPF, Adam Mayingu kwa kuwa mzalendo wa kweli na kuwezesha mikutano ya maandalizi kufanyika kwenye kumbi za mfuko huo bila malipo.

Habari Kubwa