Uteguzi kitendawili kero za walimu mbele ya JPM 

14Dec 2017
Paul Mabeja
Nipashe
Uteguzi kitendawili kero za walimu mbele ya JPM 

RAIS John Magufuli leo anatarajiwa kuzungumza na zaidi ya walimu 3,000 kutoka nchi nzima katika Mkutano Mkuu wa Taifa wa Chama cha Walimu (CWT), ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu achaguliwe mwaka 2015.

Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa   Dodoma, Augustine Njamasi, alisema jana kuwa  jambo kubwa ambalo walimu wanataka kuzungumza mbele ya  Dk. Magufuli ni kutoa kilio chao cha miaka mingi cha walimu kutopata stahiki zao kwa wakati licha ya kuwa kada hiyo imekuwa kimya.

Alisema walimu kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamikia kutopata malipo yao ambayo ni malimbikizo ya mishahara, kupanda kwa madaraja, malipo ya matibabu na malipo ya likizo.

Aidha alisema kitendo cha Rais kuhudhuria mkutano huo ni tija kubwa kwao kwa kuwa maswali yao ya muda mrefu yatapatiwa majibu sahihi na kwa wakati tofauti na miaka mingine ambayo walimu wamekuwa hawajui  ni lini watalipwa madai yao.

Njamasi aliongeza kuwa kitendo cha Rais Magufuli kukubali kukutana na walimu kitawafanya walimu kujua hatima ya maisha yao ikizingatiwa kuwa pamoja na kwamba wanafanya kazi katika mazingira magumu, wamekuwa wakifanya kazi kwa uvumilivu mkubwa. 

Alisema mpaka sasa maandalizi ya mkutano mkuu ambao utafanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Chimwaga,  yamekamilika kwa asilimia 98.

Mkutano huo utafanyika kwa mara tatu kuanzia leo huku wajumbe wa mkutano wanatarajiwa kuwa zaidi ya 3,000.Alibainisha kuwa pamoja na wajumbe hao wa CWT, pia watakuwapo wageni waalikwa ambao wataambatana na Rais ambao ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan; Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa; na makatibu wakuu wa wizara mbalimbali.

 “Pia nchi mbalimbali zimealikwa kuwakilisha nchi zao kama vyama rafiki vya walimu ambazo ni Denmark, Ireland, Canada, Afrika ya Kusini, Ghana, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Majirani zetu Zanzibar,” alisema Njamasi. 

Habari Kubwa