Utata mwanafunzi UDSM aliyetekwa

09Mar 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Utata mwanafunzi UDSM aliyetekwa

JESHI la Polisi limefungua jalada la uchunguzi wa madai ya kutekwa kwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salam (UDSM), Abdul Nondo.

mwanafunzi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salam (UDSM), Abdul Nondo akiwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Kamishna Msaidizi wa Polisi Juma Makanya.

Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Wanafunzi Tanzania (TSNP) anadai kutekwa Dar es Salaam usiku wa kuamkia juzi na watu wasiojulikana kabla ya kuonekana mkoani Iringa juzi jioni.

Awali ilidaiwa kuwa Nondo (24), alitoweka kitatanishi usiku wa kuamkia Jumatano huku viongozi wenzake katika jumuiya hiyo wakidai kuwa kabla ya kutoweka alituma ujumbe akieleza kuwa yupo hatarini.

Hata hivyo, jana Jeshi la Polisi liliwaeleza waandishi wa habari mkoani Iringa jana kuwa mwanafunzi huyo wa mwaka wa tatu katika Kitivo cha Sayansi ya Siasa na Utawala cha UDSM, aliripoti kwenye Kituo cha Mafinga wilayani Mufindi akiwa hana jeraah lolote, akidai kutekwa na watu wasiofahamika.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Kamishna Msaidizi wa Polisi Juma Makanya, alisema jeshi hilo limefungua jalada la uchunguzi ili kubaini ukweli wa tukio hilo kama kweli mwanafunzi huyo alikuwa ametekwa au ameudanganya umma.

"Kama kweli alikuwa ametekwa, tunaahidi kwamba sisi Jeshi la Polisi tukiwapata watuhumiwa sheria itachukua mkondo wake," alisema Kamanda Makanya.

Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kuchunguza kama Nondo ametoa taarifa za uongo kwa nia ovu ya kutaka kuhamasisha wanafunzi wenzake kuleta uvunjifu wa amani nchini.

Kama ni hivyo, aliahidi Kamanda Makanya, Nondo atashugulikiwa "kama wahalifu wengine".

"Kwa sasa anaonekana hali yake ni nzuri, hana majeraha, makovu yoyote na afya yake ni nzuri. Jeshi la Polisi linaendelea na upelelezi kupitia maeneo yote aliyopitia," alisema Kamanda Makanya.

Kabla ya kuenea kwa taarifa ya kutoweka kwake, Nondo alizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Jumanne na kusisitiza tamko la TSNP la Februari 18 kumtaka Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Mwigulu Nchemba ajiuzulu nafasi hiyo kutokana na kupigwa risasi na kuuawa kwa Akwilina Akwilin, lipo pale pale.

Akwilina, aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa ndani ya daladala wakati wa maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jijini Februari 16.

Kutokana na mauaji hayo, TSNP ilitoa tamko la kumtaka Waziri Nchemba kujiuzulu kuonyesha uwajibikaji kutokana na kile ambacho jumuiya hiyo ilidai katika kipindi chake cha uongozi wizarani hapo, nchi imegubikwa na matukio mengi ya mauaji na utekaji wa raia pamoja na Jeshi la Polisi kutozingatia maadili yake ya kazi.

Msemaji wa TSNP, Hellen Sisya alisema mara ya mwisho walipokuwa na Nondo UDSM, aliaga kuwa anakwenda nyumbani kwao Madale, jijini Dar es Salaam kwa sababu chuo kimefungwa lakini akapatikana Iringa.

Alisema tayari walitoa taarifa Kituo cha Polisi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kufunguliwa jalada UD/RB/1438/2018.Sisya alidai kuwa katika shughuli za mtandao ambazo zimejikita katika kutetea wanafunzi viongozi wake wamekuwa wakipokea vitisho tofauti kutoka kwa watu mbalimbali.

Habari Kubwa