Utata matibabu ya Lissu Kenya

31Dec 2017
Salome Kitomari
Nipashe Jumapili
Utata matibabu ya Lissu Kenya
  • *Wizara ya Afya yaanika msimamo wake
  • *Ni baada ya ndugu kudai kuiandikia barua

UTATA umeibuka kuhusiana na matibabu ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Baada ya ndugu kudai kuiandikia barua serikali kwa nia ya kuitaka isaidie kumgharimia huku wizara inayoshughulikia masuala ya afya ikitoa msimamo unaoashiria kuwa haihusiki moja kwa moja na jambo hilo.

Lissu aliyeshambuliwa kwa risasi zaidi ya 20 na watu wasiojulikana mchana wa Alhamisi ya Septemba 7 mjini Dodoma, alianza kutibiwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma kabla baadaye kukimbiziwa Nairobi, Kenya kwa ndege maalum ya kukodi kwa ajili ya matibabu zaidi.

Hadi sasa, Lissu bado anaendelea na matibabu nchini Kenya na ameanza kupata nafuu kulinganisha na hali aliyokuwa nayo wakati alipofikishwa nchini humo kwa mara ya kwanza.

Wiki iliyopita, Vicent Mghwai ambaye ni mdogo wa Lissu, aliiambia Nipashe kuwa gharama za kumtibia ndugu yao zinaendelea kuwa juu katika kipindi hiki anachoendelea kuhudumiwa na kwamba, wakati alipokuwa akifanyiwa upasuaji wa mara kwa mara, malipo yalifikia hadi Sh. milioni 400.   

Alisema kwa sababu hiyo, waliiandikia serikali kuomba isaidie kumtibu, akisisitiza kuwa wamefanya hivyo kufuata maelekezo kutoka kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

Waziri Ummy aliwahi kukaririwa Septemba akiwaambia waandishi wa habari kuwa serikali iko tayari kumtibia Lissu kokote duniani iwapo itapokea barua ya maombi kutoka kwa ndugu au familia, na pia mahitaji hayo yawe na baraka za madaktari.

Mdogo huyo wa Lissu alisema walilazimika kuiandikia wizara kuomba itimize ahadi ya kusaidia matibabu ya Lissu kutokana na kile alichodai kuwa kauli ya Waziri Ummy ilirudisha nyuma kasi ya wasamaria wema kumchangia ndugu yao baada ya kuaminika kuwa serikali iko tayari kumgharimia.

Hata hivyo, wakati Mghwai akizungumzia matumaini ya barua aliyodai kuwa wameifikisha serikalini, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubisya, alisema hawajawahi kupokea barua kutoka kwa familia ya Lissu kuhusiana na suala hilo.

Alipoulizwa iwapo Lissu ameshapata msaada wowote wa moja kwa moja kutoka wizarani kwake kuhusiana na matibabu anayoendelea nayo nchini Kenya, Dk. Ulisubisya alisema hakuna kwa sababu masuala yote ya matibabu kwa wabunge huwa yanashughulikiwa na Ofisi ya Bunge.

 “Kwa utaratibu wa waheshimiwa (wabunge) mambo yao yote ya matibabu yanashughulikiwa na Bunge. Kwa hiyo kama mnataka kujua mambo ya gharama, matibabu amesadiwa kiasi gani, tafadhali muwasiliane na Bunge,” alisema Dk. Ulisubisya na kuongeza:

 “Hata wale wengine (wabunge) ambao huwa tunawasaidia kwenda nje, wote wanalipiwa na Bunge kwa sababu hawaji katika fungu letu sisi (wizara).”

Dk. Ulisubisya ni mmoja wa madaktari waliomhangaikia Lissu katika kuokoa maisha yake na kumpatia matibabu ya awali Dodoma Septemba 7, mwaka huu, baada ya kushambuliwa kwake na watu wasiojulikana. Ni matibabu hayo ya Dk. Ulisubisya na wenzake ndiyo yaliyompa Lissu ahueni ya kumudu safari ya ndege kuanzia Dodoma na mwishowe Nairobi, nchini Kenya.

Hivi karibuni, Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliwaambia waandishi wa habari nyumbani kwake mjini Dodoma kuwa anatarajia kwenda kumtembelea Lissu, Nairobi nchini Kenya baada yab kumalizika kwa sikukuu za Krismasi na mwaka mpya.

Ndugai aliongeza kuwa ofisi yake ipo pamoja na Lissu na kwamba, kilichomchelewesha kwenda kumjulia hali ni hali tete ya kisiasa iliyokuwapo nchini Kenya wakati wa mchakato wao wa uchaguzi mkuu, lakini sasa hali imetulia na hivyo atakwenda kumtembelea hospitalini alikolazwa.

“Ni mbunge wetu, tunampenda na tuko naye,” Ndugai alikaririwa akisema, huku akiongeza kuwa tayari ofisi yake ilishawatuma wabunge wawili kwenda ambao ni Mary Chatanda (CCM) na Faharia Shomari (CCM).

Alisema wabunge hao ni wajumbe wa Kamisheni ya Bunge ama Tume ya Huduma za Bunge na kwamba tume (Huduma za Bunge) ndiyo inayohusika na maslahi yote ya wabunge, ikiwamo wanapofariki na kuugua na pia yenyewe ndiyo mwajiri wa wabunge.
Kuhusu maslahi ya Lissu yuanayozuingumzwa na familia yake, Nduai alikaririwa zaidi akisema kuwa alishawapa ushauri juu ya taratibu za masuala ya Serikali na Bunge.

Katikati ya wiki, ikiwa ni siku moja baada ya sikukuu ya Krismasi, Lissu alionyesha matumaini makubwa kwa wapendwa wake baada ya picha yake kusambaa mitandao mbalimbali ya kijamii ikimuonyesha kusimama kwa mara ya kwanza tangu alazwe siku 111 zilizopita huku mwenyewe akikaririwa kwa ujumbe unaoelezea namna ‘mababa cheza’ walivyomsaidia kutimiza jambo hilo.

“Leo Boxing Day (siku ya kupeana zawadi baada ya Krismasi) nimeweza kusimama kwa mguu mmoja kwa msaada wa ‘mababa cheza’ kama inavyoonekana. Hatua inayofuata nitawajulisha accordingly,” taarifa hiyo iliyosambazwa na msemaji wa Lissu, Hemed Ali, ilieleza kwa kunukuu maneno ya mbunge huyo ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

Hatua hiyo ya Lissu kusimama iliwashangaza wengi ambao waliamini kuwa angemudu kusimama au kutembea baada ya kufikiwa kwa hatua nyingine ya matibabu nje ya Kenya, ambayo yangehusisha kufanya mazoezi maalum na hatua hiyo ilitarajia kufanyika mwakani.

 
 

Habari Kubwa