Upungufu madaktari, wauguzi unavyotesa

17Jul 2017
Godfrey Mushi
Nipashe
Upungufu madaktari, wauguzi unavyotesa

SEKTA ya afya katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi iko katika wakati mgumu kutokana na kukabiliwa na upungufu madaktari na wauguzi zaidi ya 152.

waziri wa afya, ummy mwalimu.

Hayo yamo katika taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo, Michael Mwandezi aliyoitoa juzi wakati wa kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani.

“Sekta ya afya inakabiliwa na upungufu wa wauguzi na matabibu zaidi ya 152 ambao ni kati ya watumishi 619 wanaohitajika," alisema Mwendezi na kueleza "kimsingi bado tunasubiri kibali cha serikali kwa ajili ya kuajiri.”

Kuhusu vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano, Mwandezi alisema kwa mwaka wa fedha uliomalizika wa 2016/2017, vilikuwa 19 kati ya vizazi hai 1,000.

Pia alisema vifo vya watoto wachanga 33, kati ya 1,000 ambao huzaliwa katika vituo vya afya na hospitali zilizopo Manispaa ya Moshi hutokea kutokana na sababu mbalimbali, na kuwa idadi ya wanawake wanaojifungua kwenye vituo afya ni asilimia 99.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, huduma za uzazi wa mpango katika Manispaa ya Moshi zinatekeleza kwa asilimia 52.

Aidha, Mwandezi alisema maambukizi ya ugonjwa wa malaria katika Manispaa hiyo ni asilimia tano na maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi ni asilimia 2.5 ya wakazi wa Manispaa ya Moshi.

Pamoja na mambo mengine, Mwandezi alieleza suala la upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi bado ni changamoto kubwa kwao.

“Mpaka kufikia Desemba 31 mwaka jana, hali ya upatikanaji wa dawa muhimu katika utoaji wa huduma za afya ulikuwa wastani wa asilimia 71 na mwezi Januari mwaka huu, tumeweza kupata dawa za kutosha, lakini suala la upatikanaji wa dawa na vifaa tiba uko kwa asilimia 85,” Mwandezi alisema.

Habari Kubwa