Upinzani wasuasua kampeni

03Jan 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Upinzani wasuasua kampeni

WAKATI muda wa kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Songea Mjini mkoani Ruvuma zimeshaanza rasmi kwa mujibu wa ratiba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) pekee ambacho kimeanza kunadi mgombea wake.

Vyama vingine ambavyo vimesimamisha wagombea, hakuna hata kimoja kilichoanza kampeni kwa ajili ya kunadi wagombea na sera zao.

Katika uchaguzi huo wa kujaza nafasi ya aliyekuwa mbunge, Leonidas Gama (CCM), baada ya kufariki dunia, ni chama tawala ambacho kinaendelea kumnadi mgombea wake, Dk. Damas Ndunbaro.

Kampeni hizo za CCM zilizinduliwa Desemba 30, mwaka jana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, katika Kata ya Lizaboni mjini Songea ambapo pamoja na kuzindua kampeni hizo, pia aliwataka wananchi kujitokeza kujiandikisha kwa ajili ya kupata vitambulisho vya uraia kwani muda ukiisha hatua zitachukuliwa kwa yeyote ambaye hatakuwa na kitambulisho hicho.

Naye Dk. Ndumbaro akijinadi na kuomba kura katika kata za Lilambo na Ruhuwiko, aliahidi kuendelea kutekeleza ilani ya CCM na kuvitaja baadhi ya vipaumbele vyake kuwa ni elimu, afya na kilimo.

 

Habari Kubwa