Upasuaji wa kwanza wa kongosho wafanywa KCMC

08Mar 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Upasuaji wa kwanza wa kongosho wafanywa KCMC

UPASUAJI wa kwanza wa njia ya matundu wa kuondoa mawe katika mfuko wa kongosho, umefanyika katika Hospitali ya Rufani ya KCMC ya Moshi, ukihusisha jopo la madaktari bingwa wa upasuaji kutoka nchini Uingereza na mikoa ya Kanda ya Kaskazini, Tanzania.

kongosho

Upasuaji huo wa mafanikio uliongozwa na daktari bingwa wa upasuaji wa hospitali hiyo, Dk. Kondo Chilongela, pia ulimhusisha mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa kada hiyo, Dk. Theresia Mwakyembe.

Akizungumza jana baada ya upasuaji huo, Dk. Kondo, alisema aina hiyo ya upasuaji inatajwa kupunguza muda wa kufanyika operesheni pamoja na mgonjwa kukaa muda mrefu hospitalini akiuguza vidonda.

“Tumepata mafanikio makubwa katika upasuaji huu, madaktari bingwa kutoka mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Tanga na baadhi ya mikoa ya Kanda ya Kati, kwa kushirikiana na madaktari bingwa kutoka Northumbria, Uingereza, wameshiriki upasuaji wa kwanza wa kuondoa mawe kwenye kongosho kwa njia ya matundu,” alisema Dk. Kondo.

Akizungumzia ushiriki wake, Mwakyembe, mwanafunzi wa mwaka wa tatu anayesomea upasuaji katika Chuo Kikuu Kikishiriki cha Tiba na Uuguzi cha KCMC, alisema amefurahi namna magwiji hao walivyomwelekeza hatua za kufuatwa wakati operesheni zinapofanyika.

Dk. Mwakyembe alisema: “Ni furaha sana kwangu kuwa mwanafunzi wa kwanza nchini Tanzania kushiriki upasuaji wa aina hii ambao ndio kwanza unaanza kufanyika katika nchi za Afrika. Nilichojifunza ni kwamba upasuaji huu unamwezesha mgonjwa kupona kwa muda mfupi, kutopata jeraha kubwa na kutoongezewa damu.” 

Habari Kubwa