Uhaba wa watumishi waathiri huduma afya 

03Jan 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Uhaba wa watumishi waathiri huduma afya 

WAKAZI wa Kijiji cha Chipwa wilayani Kalambo mkoa Rukwa, wameiomba serikali ya mkoa kuwaongeza watumishi katika zahanati ya kijiji, ili kuondoa ukosefu wa huduma za afya unaojitokeza. 

mkuu wa mkoa wa rukwa, Joachim Wangabo.

Ombi hilo walilitoa  kwa mkuu wa mkoa huo, Joachim Wangabo, wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika kijiji hicho akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili wilayani humo. 

Akizungumza kwa niaba ya wakazi hao, Peter Sichone, alisema kuwa zahanati ya kijiji hicho kilichopo mwambao wa Ziwa Tanganyika mpakani na Zambia, ina wahudumu wawili hivyo kukabiliwa na changamoto ya utoaji huduma kwa kuwa watumishi ni wachache. 

Alisema hivi sasa mtumishi mmoja yupo likizo na mwingine anapokwenda kuchukua mshahara wilayani ama akiugua zahanati hiyo inafungwa, hivyo wananchi wanalazimika kusafiri kwa njia ya maji kufuata huduma katika zahanati nyingine na wakati mwingine kuvuka ziwa na kwenda Zambia kutafuta matibabu.

“Kwa kweli tunahangaika sana kupata huduma za afya kutokana na kuwa watumishi hawatoshi wapo wawili tu, hivyo tunalazimika tukisafiri kwenye maji umbali mrefu kutafuta huduma, tunatumia usafiri wa mitumbwi ambao sio salama na wakati mwingine tunashindwa kwa kuwa ziwa linakuwa na dhoruba na mawimbi makubwa na maboti tunayosafiria siyo salama,” alisema. 

Habari Kubwa