Tuhuma ujangili wa tembo kuchunguzwa

03Jan 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Tuhuma ujangili wa tembo kuchunguzwa

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Mpango wa  Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Natalie Boucly,-

Wamekubaliana kuanzisha kikosi kazi cha pamoja cha kuchunguza tuhuma zilizotolewa hivi karibuni na kituo cha televisheni cha Uingereza kuhusu ujangili wa tembo katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha iliyopo mkoani Iringa.

Dk. Kigwangalla na Mkurugenzi huyo, walifikia makubaliano hayo jana wakati wa mazungumzo yaliyofanyika katika ofisi ndogo ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Mpingo House jijini Dar es Salaam.

Aidha, Waziri Kigwangalla alimweleza Mkurugenzi huyo kuwa, Wizara yake inaandaa mikakati mbalimbali ya kuongeza idadi ya watalii nchini na mapato ikiwamo kuwashirikisha wananchi kuandaa mwezi maalum wa Urithi wa Tanzania pamoja na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato kwa njia za kielektroniki katika vituo mbalimbali vya utalii.

Kwa upande wake, Mkurugenzi huyo alimuahidi Waziri Kigwangalla kuendelea kumpa ushirikiano katika nyanja mbalimbali za kuendeleza utalii nchini na uhifadhi wa misitu na wanyamapori kwa ujumla. 

Habari Kubwa