TCRA yaonya watoto kusajili laini za simu

18Nov 2017
Rahma Suleiman
Nipashe
TCRA yaonya watoto kusajili laini za simu

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), hairuhusu watoto wenye umri chini ya miaka 18 kusajili laini za simu.

Mkurugenzi wa masuala ya watumiaji na watoa huduma wa TCRA, Raymold Mfungahoma, akizungumza na waandishi wa habari visiwani Zanzibar.

Mkurugenzi huyo, alisema vitambulisho vinavyotumika katika usajili wa laini za simu ni vile ambavyo mtumiaji wa simu ana umri wa zaidi ya miaka 18.

“Ni bahati mbaya kwamba kama wazazi au walezi hatutekelezi wajibu wetu tunawachia simu watoto ni hatari hawajafikia umri wa kutumia bidhaa hizi ”alisema Mkurugenzi.

Aliwataka wazazi na walezi kuwadhibiti watoto kutotumia simu hasa kuangalia picha ambazo hazina maadili.

Alisema ni vyema mzazi au mlezi kuchukua wajibu wake kumlinda mtoto ili asiathirike kutokana na mambo yaliyo ndani ya simu kwa kuwa bado hawajakomaa.

Alisema watoto wapo katika hali ya hatari hivyo wazazi wasipowaelekeza watoto athari za matumizi ya mawasiliano anaweza akaharibikiwa kwa kuangalia mambo ambayo hayaendani na maadili.

“Mtoto anaharibikiwa akiwa mdogo kwa kuangalia vitu ambavyo havifai inamvuruga akili na baadaye anaona kama ni sawa hivyo kila mtu ajaribu kusaidia, kumuelimisha mtoto kujua kati ya picha nzuri na picha mbaya,”alisema.

Hata hivyo, alisema mzazi anawajibika kwa malezi ya mtoto kuhusiana na masuala ya mawasiliano na kama mzazi anahitaji mtoto wake awe na simu ni vyema kusajili laini ya simu kwa jina la mzazi lakini pia kuchukua nafasi ya kumuelewesha mtoto kuhusu matumizi sahihi ya mitandao ya mawasiliano.

Habari Kubwa