Tani 16 sangara zilivyokamatwa

03Jan 2018
Lilian Lugakingira
Nipashe
Tani 16 sangara zilivyokamatwa

SERIKALI wilayani Muleba mkoani Kagera, imekamata tani 16 za samaki aina ya sangara, waliovuliwa na kukaushwa kinyume cha sheria.

Kwa mujibu wa mkuu wa wilaya ya Muleba, Richard Ruyango, samaki hao walikamatwa katika kisiwa cha Rubili Kata ya Mazinga wilayani humo, kufuatia msako wa kushtukiza uliofanywa na uongozi wa Wilaya ya Muleba.

 

Ruyango alisema kuwa samaki hao walikamatwa Januari mosi, mwaka huu, kutokana na kukiukwa kwa Sheria ya Uvuvi Namba 22 ya mwaka 2003, inayokataza kuchakata samaki bila ya kuwa na leseni ya uvuvi.

 

Mkuu huyo wa wilaya katika operesheni hiyo ya kushtukiza alifuatana na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya, hadi katika eneo la tukio, na kuwakuta samaki hao wakiwa wanakaushwa juani na wengine wakiwa wamepakiwa katika magunia, tayari kusafirishwa nje ya nchi.

 

Alisema  mmoja wa watu waliokutwa akisimamia zoezi hilo aliyejulikana kwa jina moja la Salum, alidai  si mmiliki wa mzigo huo, na anashikiliwa kwa tuhuma za kupatikana na samaki hao.

 

Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo husika dhidi ya vitendo vya uvuvi haramu, vinavyoendelea katika visiwa mbalimbali wilayani hapa, ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.

 

Kwa upande wake Kaimu Ofisa Mfawidhi wa Kikosi cha Doria na Udhibiti Uvuvi Kanda ya Kagera, Ernest Kazimili, alisema walifanya msako katika kaya mbalimbali na kufanikisha kuwakamata samaki hao.

 

Aidha, Kazimili aliwataka wananchi kuacha shughuli za uvuvi haramu, kwani ni kinyume cha taratibu na sheria za nchi.

 

 

 

 

Habari Kubwa