Sumatra yaibua madudu barabarani  

31Dec 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Sumatra yaibua madudu barabarani  

MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Maji na Nchikavu (Sumatra) mkoani Kagera imeeleza kuwa kuna  ukiukaji mkubwa wa sheria na taratibu unaofanywa na magari ya abiria.

Hayo yalisemwa na Ofisa Leseni mkoani Kagera, Shadrack Mlale, baada ya kutembelea Wilaya za Ngara na Biharamulo na kuona jinsi madereva wanavyokiuka matumizi ya barabara walizopangiwa sambamba na kuongeza nauli bila kuzingatia maelekezo na bei za mamlaka.

 

"Tumetembelea wilaya mbili pekee katika mkoa huu ambao zinaingiliana na mikoa mingine na kubaini ukiukaji wa taratibu za Sumatra kwa baadhi ya magari yasiyo stahili kufanya safari zake kwenye wilaya hizo,"alionya Mlale.

 

"Yamekuwa ni mazoea yao na hiyo inatulazimisha  kuwapiga faini kwa  vitendo na mabaya yao na kuwarudishia nauli  abiria "alisema Mlale.

 

Alisema kazi hiyo itakuwa endelevu kuona kama madereva wengine katika stendi ya Bukoba mjini ambako magari mengi kutoka kwenye mikoa mingine huingia kuleta na kubeba abiria ili kuona kama wanafuata taratibu.

 

Aidha, alisema tayari chapa za Sumatra zimeshabandikwa maeneo ya stendi ili kusaidi abiria kutambua nauli inayotakiwa kutolewa anakokwenda.

 

Joseph Msato,  dereva anayesafiri kati ya  Mwanza na Bukoba alisema suala la upandishwaji nauli limekuwepo kwa kiwango kidogo  kwa baadhi ya mabasi yaendayo mikoa kwa mikoa.

 

Msato alisema kiasi cha fedha kilichoongezwa ni Shilingi 1,000-2,000 lakini kuna magari mengine yanatoza nauli pungufu.

 

Abiria wa magari yaendayo Mwanza Adelida Msana alisema kadri siku zinavyosogea hasa katika nyakati za sikukuu ongezeko la nauli linapanda na hii husababishwa na wingi wa abiria na magari kuondoka mapema.

Habari Kubwa