Sheria kufunga mateja miaka 30 yatinga rasmi

18Nov 2017
Sanula Athanas
Nipashe
Sheria kufunga mateja miaka 30 yatinga rasmi

BUNGE limepitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ambao imependekeza adhabu kali zaidi ikiwamo ya kifungo cha maisha gerezani ili kukomesha mtandao wa wanaojihusisha na biashara hiyo haramu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama.

Mbali na kifungo vya maisha gerezani, muswada huo unapendeza kutaifisha mali za wanaojihusha na biashara hizo huku maofisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya wakiruhusiwa kumiliki na kutumia silaha za moto katika kukabiliana na wauzaji wa dawa hizo.

Adhabu ya kifungo cha maisha gerezani, kwa mujibu wa muswada huo, ni kwa wanaowaweka rehani watu ili kufanikisha biashara ya dawa za kulevya, wamiliki wa mitambo ya kutengeneza dawa hizo na watakaowaingiza watoto kwenye matumizi na biashara ya dawa za kulevya.

Imeelezwa kuwa kabla ya marekebisho hayo, sheria hiyo ilikuwa na upungufu katika utekelezwaji wake ikiwamo kutoa adhabu ndogo iliyowafanya baadhi ya wahusika kupata mwanya wa kuendeleza biashara ya dawa za kulevya.

Akiwasilisha muswada huo bungeni mjini hapa jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, alisema atakayetiwa hatiani kwa kosa la kusafirisha mirungi au bangi zaidi la kilo 50, pia atahukumiwa kifungo cha maisha gerezani.

Alisema masuala ya msingi yaliyozingatiwa kwenye muswada huo ni kuharamisha baadhi ya vitendo, kuweka adhabu, kuidhinisha vigezo vya kufuata wakati wa utoaji dhamana na uwezo wa mahakama katika kusikiliza mashauri yanayotokana na sheria hiyo.

Mhagama alisema kifungu cha 15(1) cha muswda huo kimependekezwa kuongezwa kipengele (C) ili kuweka katazo la kuwezesha au kusababisha mtu kusafirishwa nje ya nchi kuwekwa rehani ili kufanikisha biashara ya dawa za kulevya.

"Kipengele hiki kinaweka adhabu ya kifungo cha maisha kwa mtu atakayekiuka masharti ya kifungu hicho. Vilevile kifungu kidogo cha pili kimerekebishwa kwa kuzuia yeyote kujihusisha isivyo halali na kemikali zinazotumika kutengenezea dawa za kulevya.

"Kifungu cha 29, marekebisho yamelenga kuongeza makosa yasiyostahili dhamana ambayo yatajumuisha makosa ya kumiliki mitambo ya kutengenezea dawa za kulevya, kufadhili na kuwaingiza watoto kwenye matumizi na biashara ya dawa hizo," alifafanua.

Waziri huyo alibainisha kuwa misingi wa mapendekezo hayo ni kudhibiti ongezeko la wafanyabiashara wakubwa, kupunguza utunzaji na usambazaji dawa za kulevya.

SILAHA ZA MOTO

Mhagama alibainisha kuwa kifungu kipya cha 40(A) kimeongezwa kwa lengo la kuweka masharti kwa maofisa wa mamlaka hiyo kumiliki na kutumia silaha za moto pale inapobidi.

Alisema msingi wa marekebisho hayo unatokana na ukweli kwamba, wafanyabiashara wa dawa hizo wana nguvu kubwa za kifedha ambazo huwawezesha kumiliki silaha na kujiwekea kinga ya ulinzi wakati wote.

Kutokana na hali hiyo, Mhagama alisema maofisa wa mamlaka hiyo wanajiweka kwenye mazingira hatarishi wakati wa ukamataji.

"Mamlaka imekuwa ikiwatumia polisi kwa ajili ya ulinzi wakati wa kufanya operesheni za kuwakamata watuhumiwa. Wakati mwingine taarifa zinapatikana usiku na kuhitaji utekelezaji wa haraka," waziri huyo alisema na kufafanua zaidi:

"Hali hiyo huwalazimu maofisa kujitoa muhanga na kuhatarisha maisha yao au ukamataji, hivyo kutoa mwanya kwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya kuendelea kufanya biashara kwa uhuru."

Alisema lengo la uamuzi huo ni kuiwezesha mamlaka kutekeleza majukumu ya kukamata, kupekua, kuazia mali na vielelezo vya watuhumiwa na kuhakikisha usalama wa watendaji wake.

UTAIFISHAJI
Kuhusu utaifishaji wa mali za wafanya biashara wa dawa za kulevya, Mhagama alisema kifungu cha 49(1) kilikuwa kikizungumzia kutaifisha mali zilizopatikana siku ya kutiwa hatiani au baada ya hapo.

Alisema athari ya kifungu hicho ni kuwa hakihusishi mali zilizopatikana kabla ya kutiwa hatiani kwa mtuhumiwa na zile za washirika wake katika biashara ya dawa za kulevya.

Hivyo, alipendekeza kuwa kifungu kidogo cha kwanza cha kifungu hicho kifutwe na kuandikwa upya ili mali itakayotaifishwa iwe iliyopatikana siku ambayo mtuhumiwa alishitakiwa na si tarehe aliyotiwa hatiani.

Mhagama pia alitaka kifungu kidogo cha nne cha kifungu hicho kimeandikwa upya kwa lengo la kuongeza muda wa kutaifisha mali kutoka miaka mitano hadi 10 nyuma ya tarehe ya kushitakiwa.

Waziri huyo alibainisha kuwa kifungu kipya cha 51(A) kimeongezwa kwa lengo la kumpa uwezo Kamishna Jenerali wa mamlaka hiyo kushikilia akaunti za benki za watuhumiwa.

Alisema lengo la kufanya hivyo ni kuimarisha na kuboresha taratibu za uchunguzi na kuweka uhakika wa fedha haramu kutotoroshwa kwa urahisi au uchunguzi kuharibiwa.

"Sheria iliyopo haimpi uwezo Kamishna Jenerali  kuweka zuio au kushikilia akaunti za benki za watuhumiwa hivyo kuathiri utendaji kazi wa mamlaka na kuongeza mwanya kwa watuhumiwa kutorosha au kuhamisha fedha wakati wa uchunguzi," alisema.

Mapendekezo mengine yaliyomo kwenye muswada huo ni kwenye kifungu cha 55(1) ambacho kimeweka utaratibu wa kufanya makubaliano kati ya Tanzania na nchi za nje kusaidia kutaifisha, kubaini au kukamata mali kwa minajili ya kutaifisha.

VIROBA
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi kuhusu muswada huo, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk. Jasmine Bunga, alisema serikali inapaswa kuona umuhimu wa kuongeza pombe aina ya viroba na dawa zingine za binadamu zinazotumika kama dawa za kulevya kwa sehemu ya dawa zinazolengwa na muswada huo.

Alisema kuna umuhimu kwa Tanzania Bara na Zanzibar kutafuta mbinu ya kudhibiti mianya ya kupenyesha dawa za kulevya kwa kuwa sheria itakayotungwa kutokana na muswada itatumika Tanzania Bara pekee.

Dk. Jasmine alisema kamati yake pia imeitaka Mamlaka ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya, kuhakikisha inadhibiti ripoti za uchunguzi ulioaninishwa chini ya sheria hiyo kuondoa mazingira ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuwabambikizia watuhumiwa kesi kwa kutumia ripoti zilizogushiwa.

Katika maoni yake, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kupitia kwa msemaji wake kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu, Masoud Abdallah Salim, ilionyesha wasiwasi kuhusu maofisa wa mamlaka kupewa ruhusa kutumia silaha.

"Kitendo cha kuruhusu maofisa hao ambao haijaelezwa kwenye muswada kama wanayo mafunzo ya kukamata au kushughulika na wahalifu kama vile askari na maofisa usalama, kinatia wasiwasi," alisema.

"Ofisa anapopewa mamlaka makubwa ya kutumia silaha ni hatari kwa usalama wa raia hasa pale atakapotumia silaha hizo kinyume cha sheria," aliongeza Salim.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Lucy Mayenga, akichangia muswada huo, alipongeza juhudi za Rais Dk. John Magufuli katika kuongoza mapambano dhidi ya biashara ya dawa za kulevya.

Pia aliitaka mamlaka ya kupambana na dawa hizo visiwani Zanzibar kuongeza jitihada kwa kuwa tangu ilipoanzishwa miaka 10 iliyopita, haijawahi kukamata hata kilo tano za dawa za kulevya.

Naye Riziki Lulida, Mbunge wa Viti Maalum (CUF), alitaka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), kumulikwa kwa makini hususani kwenye jengo la watu mashuhuri (VIP).

Alisema jengo hilo limekuwa njia ya kupitishia washukiwa wa dawa za kulevya kwa kuwa idadi kubwa ya watu wasiokuwa na hadhi hiyo, hupita bila kufanyiwa uchunguzi wa kina.

"Wengine wanapita VIP bila kukaguliwa na wakati mwingine mgonjwa aliye kwenye kiti cha magurudumu, utashuhudiwa akisindikizwa na watu zaidi ya wanne wakiwa na mabegi," alieleza.

Mbunge huyo pia aliitaka serikali kuongeza kasi ya kufanya doria kwa kudhibiti njia za panya hususan ukanda wa pwani ambako mikoa ya kanda hiyo ndiyo imeathirika zaidi kwa matumizi ya dawa za kulevya.
 

Habari Kubwa