Shein ashtukia wana-CCM Z'bar

12Jan 2017
Salome Kitomari
Nipashe
Shein ashtukia wana-CCM Z'bar

RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, ameonya wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wanaojinadi chinichini kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao kuacha kufanya hivyo.

Akizungumza katika mahojiano maalumu ya maadhimisho ya miaka 53 ya mapinduzi ya Zanzibar na Televisheni ya Azam, Rais Shein alisema wanaotamani uraisi wajue muda bado.

Chama kitatoa tarifa na kutangaza mwenye nia ya kugombea kiti hicho ajitokeze kuchukua fomu, alisema Rais Shein.

"Anayefanya utaratibu wake wowote anakwenda kinyume na katiba ya CCM, maadili ya uongozi na chama," alisema Rais Shein ambaye kipindi chake cha uongozi kitakoma mwaka 2020.

“Wavute subira tu, bado nina miaka minne mbele."

Pamekuwa na harakati za chini kwa chini za baadhi ya wanachama wa CCCM ambao wamekuwa wakipita katika matawi kujiuza.

"Mambo hayaendi kwa kujificha ficha, kwa jazba," alisema Dk. Shein. "Ngoja wakati ufike watagombea urais kwa taratibu zilizopo.
“Nafasi ya uongozi si ya mapenzi ya mtu, nafasi ya uongozi ni maamuzi ya chama.

"Hata kama nampenda mtu sana, sina mamlaka ya kumnong’oneza au kumpendekeza bali Kamati Kuu (ya CCM), Halmashauri Kuu ya Taifa… chama kikimteua nitamuunga mkono.”

Aidha, Rais Shein alisema kihulka yeye ni mpole lakini huwa havumilii uzembe na kutokuwajibika kwa namna yoyote.

”Mimi sipendi kusemasema sana… upole ni udhaifu nilionao, utaratibu ni sifa, lakini siwezi ona mtu anaharibu nchi (nikabaki) namtazama tu," alisema.

"Nitamshughulikia.
“Napenda kupima mambo, napenda kutumia busara sana, ni sifa yangu, lakini mtu akiharibu kazi simwachii; nitamchukulia hatua.”

MAALIM SEIF
Alipoulizwa kama harakati za Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad kupaza sauti ndani na nje ya nchi kupinga uchaguzi wa marudio wa Zanzibar wa Machi 20, mwaka jana ambao ulimuingiza madarakani zimeshitua, Rais Shein alisema:

“Sijashtuka na wala sitashtuka kwa sababu uchaguzi uliendeshwa kwa halali, kwa katiba na kwa mujibu wa sheria.

“Hakuna mtu mwenye mamlaka yoyote na uchaguzi wa Zanzibar kama siyo chombo cha usimamizi kama Tume ya Uchaguzi (ambayo) haiingiliwi na Mahakama yoyote duniani.

"Hata kama akienda kushtaki, Tume imeshatangaza mshindi; hakuna mahakama yoyote duniani inaweza kutengua.”

Maali Seif alikuwa mpinzani wa Dk. Shein katika kiti cha urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015 ambao ulifutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Salim Jecha.

Jecha alifuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu kwa madai ya kuwapo kwa kasoro zilizoufanya usiwe wa haki.

UWEZO WAKE
Alipoulizwa juu ya utendaji kazi wa Rais John Magufuli, Dk. Shein alisema anaridhishwa na kasi yake na kwamba amemfahamu kwa miaka tisa aliyofanya kazi Bara akiwa Makamu wa Rais na Magufuli akiwa Waziri wa Ujenzi na baadaye Waziri wa Uvuvi.

“Namjua uwezo wake na namjua staili yake ya uongozi," alisema.

"Kila kiongozi ana muundo wake wa kuongoza, uongozi unategemea unaongozwa na nani na wale unaowaongoza, alimradi unakuwa ndani ya sheria, Katiba na taratibu.”

Alibainisha hata yeye amekuwa akitumbua majipu, na kwamba hufanya kimya kimya.

Alisema watumishi 12 wameshatumbuliwa na wengine wanachunguzwa kwa rushwa.

Aidha, Rais Shein alisema anajivunia elimu bure aliyoianzisha na kwamba kwa sasa wanaboresha taaluma kwa kuhakikisha kunakuwa na walimu wa kutosha na miundombinu.

Upande wa afya alisema huduma zimeboreshwa na kwamba kuna vituo vya afya 154 kutoka 36 zilivyokuwapo na kwamba hospitali zimeongezeka mara tatu zaidi.

Kuhusu utalii, alisema sera na sheria zimebadilika na kuwataka wawekezaji na mawakala wa utalii kufanya shughuli hizo visiwani humo ili fedha iendelee kuwapo, tofauti na miaka ya nyuma fedha ilibaki Ulaya.

Alisema kuna hoteli 27 za nyota tano Zanzibar na nyingine nyingi za nyota nne na tatu.

Habari Kubwa