Serikali yashtuka ukubwa deni la walimu

21Apr 2017
Gwamaka Alipipi
Nipashe
Serikali yashtuka ukubwa deni la walimu

KASI ya ongezeko la madeni ya walimu imeishtua serikali na kueleza kuwa kutokana na hali hiyo, imeanza kuchukua hatua madhubuti za kudhibiti ikiwamo kuanza kulipa.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema hayo bungeni mjini hapa jana alipokuwa akijibu swali la Venance Mwamoto (Kilolo-CCM) aliyetaka kujua mikakati ya serikali katika kulipa malimbikizo ya deni ya walimu.

“Walimu wanalia kuna malimbikizo makubwa ya madeni yao wanayodai kwa muda mrefu. Je, nini kauli ya Serikali katika kuhakikisha madeni hayo yanalipwa na kuwapa motisha walimu kufanya kazi vizuri?” alihoji.

Katika kujibu swali hilo, Waziri Mkuu alisema ni kweli Serikali inadaiwa na watumishi wa umma, wakiwamo walimu, lakini mikakati ya kulipa madeni hayo imeanza.

“Ni kweli walimu wanaidai serikali na itamaliza madeni hayo kwa watumishi wa serikali na tumeanza kuyapitia madeni hayo. Madeni ya walimu yameshakusanywa na yamehakikiwa na wakurugenzi wa halmashauri,” alisema Waziri Mkuu.

Alisema Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) nayo pia imeshakagua ili kuona uhalali wa madeni hayo baada ya kuona yamekuwa makubwa.

Alisema serikali imeanza kuweka utaratibu wa kuweka utaratibu wa kudhibiti ukuaji wa madeni hayo na kwamba baadhi ya madeni ambayo hayana kiwango kikubwa yameanza kulipwa na halmashauri. Alitoa  mfano wa Halmashauri ya Arusha ambayo imeanza kulipa madeni ya watumishi wake wa ndani zaidi ya Sh. milioni 100.

WIZI WA KOROSHO

Naye Mbunge wa kuteuliwa, Salma Kikwete, alisema kuna upotevu wa Sh. bilioni 30 katika zao la korosho hivyo serikali inapaswa kuweka mikakati katika kudhibiti hali hiyo.

Akijibu hoja hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa alisema  ni kweli kuna ubadhirifu mkubwa katika mazao makuu ya biashara na siyo katika zao la Korosho peke yake.

“Vyama vya ushirika nchini vimeanza kuonyesha mwenendo usio mzuri kwani kuna upotevu mkubwa wa fedha hali inayosababisha wakulima kukata tamaa. Serikali imeanza kupitia mapitio kwa mazao yote makubwa na tumeanza na zao la korosho,” alisema Majaliwa.

Alisema serikali ilianza kukagua katika vyama vya ushirika na kwamba awali  ikabainika kuna ubadhirifu wa Sh. bilioni sita na kwamba ikabainika hasara hiyo haikutokana na Bodi ya Korosho bali ilisababishwa na vyama vikuu na vyama vya ushirika vilivyopo katika vjiji na kata.

Waziri Mkuu alisema hatua kadhaa zimechukuliwa kwa watendaji waliohusika katika ubadhirifu huo kwa  vyama vya msingi na vikuu, na hatua zingine zinaendelea kuchukuliwa.

Alisema uchunguzi bado unaendelea, na pindi utakapokamika hatua kali zitachukuliwa na moja ya  hatua ni kuwarejeshea fedha wakulima.

Habari Kubwa