Sababu Wazanzibari kuona Wachina ndugu

17Jul 2017
Rahma Suleiman
Nipashe
Sababu Wazanzibari kuona Wachina ndugu

KITENDO cha Serikali ya China kujitolea kwa dhati katika kuiunga mkono Tanzania na Zanzibar katika kusaidia taaluma na huduma kwenye sekta ya afya, ndiyo sababu ya Wazanzibari kuwaona Wachina kama ndugu, imeelezwa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.

Sababu hiyo ilibainishwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi alipokuwa akihojiwa na Televisheni ya Taifa ya China (CCTV) mjini hapa juzi.

Katika mahojiano hayo Balozi Seif aliipongeza Serikali ya China kwa uamuzi wake wa kujitolea kwa dhati wa kusaidia sekta ya afya kwa ujumla nchini na Zanzibar.

Alisema mchango wa China katika sekta hiyo umewezesha wananchi walio wengi kuhisi wataalamu na madaktari wa Kichina wanaotoa huduma za afya nchini ni ndugu zao wanaoshirikiana katika maisha ya kawaida mitaani.

Wanahabari wa CCTV wapo Zanzibar kufanya kipindi maalum kinachohusu historia ya madaktari wa China wanaotoa huduma za afya Zanzibar kwa takribani miaka 53 iliyopita.

Alisema wananchi wa Zanzibar kwa kipindi kirefu wamekuwa na ukaribu na madaktari wa Kichina kutokana na wataalamu hao mahiri katika utendaji kazi kuzingatia zaidi maadili yaliyowawezesha kujenga sifa na heshima kubwa.

Aliwahakikishia wanahabari hao kwamba Serikali ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na China katika kuona malengo ya ushirikiano yaliyofikiwa kati ya pande hizo mbili karibu miaka 53 iliyopita yanafanikiwa ipasavyo.

Akizungumzia ushirikiano wa kiuchumi na kijamii uliopo kati ya China na Bara la Afrika, Balozi Seif alisema umeshaanza kuleta mafanikio.

Alisema ushirikiano huo umesaidia kuibua wataalamu wazawa katika mataifa hayo ambao wameanza kusaidia nguvu za uzalishaji unaozingatia teknolojia ya kisasa.

Balozi Seif alifahamisha kwamba miradi ya maendeleo, hasa katika sekta za miundombinu ya mawasiliano, afya, kilimo, utamaduni, michezo na hata shughuli za kijamii chini ya usimamizi wa mabingwa na wataalamu wa China imeanza kushuhudiwa ikipiga hatua kubwa za maendeleo.

Hata hivyo, Balozi Seif aliielezea timu hiyo ya CCTV kwamba China bado ina safari ndefu ya kuendelea kulisaidia kitaaluma Afrika katika azma ya bara hilo kujikomboa na umaskini, hasa kwa mataifa yaliyo kusini mwa Jangwa la Sahara.

Habari Kubwa