RIPOTI MAALUM Ahueni wakulima tumbaku

31Dec 2017
Neema Sawaka
Nipashe Jumapili
RIPOTI MAALUM Ahueni wakulima tumbaku
  • *Mavuno ya ziada yapata wanunuzi kwa   bei nafuu walau kuwapunguzia hasara

HATIMAYE kilio cha muda mrefu cha wakulima wa tumbaku wa Kahama waliokuwa na shehena kubwa ya zao hilo kwenye maghala kutokana na ukosefu wa soko, kimepata jawabu baada ya kuwapata wanunuzi.

Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Wakulima Mkombozi kilichopo Ushetu, Kahama mkoani Shinyanga, Abdallah Shilinde (kushoto) akiwa ghalani katika siku ya kuuza tumbaku iliyokuwa imekosa wanunuzi hivi karibuni. (Picha: Neema Sawaka) 

Kwa miezi kadhaa sasa, wakulima wa zao hilo katika mkoa maalum wa tumbaku wa Kahama, walijikuta gizani baada ya neema ya mavuno ya ziada waliyoyapata katika msimu wa 2016/2017, kugeuka shubiri kutokana na ukosefu wa wateja.

Hali hiyo iliwahi kuripotiwa na Nipashe baada ya kufanya mahojiano maalum na baadhi ya wakulima, wakiwamo Regina  Ndega, Zena Magese na Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Wakulima Mkombozi kilichoko Ushetu, Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga. 

Wote walielezea pigo kubwa kiuchumi walilolipata baada ya kutumia fedha nyingi kuwekeza katika kuzalisha tumbaku ya msimu uliopita kwa matarajio ya kujikwamua zaidi kiuchumi lakini mwishowe, wengi wao wakajikuta wakielemewa madeni makubwa yakiwamo ya posho za vibaru na pembejeo mbalimbali walizozitumia wakati wa maandalizi ya shamba na pia gharama za kuvuna na kuendelea kuhifadhi zao hilo.

Katika taarifa hiyo Nipashe, ilielezwa kuwa neema ya mavuno makubwa ya tumbaku iliyowezesha kupatikana kwa tani   kilo  milioni 14.7 nchini kote, ndiyo chanzo cha kukosekana soko baada ya wanunuzi kudai kuwa hawakujiandaa kununua tumbaku ya ziada katika msimu huo.

Hata hivyo, matumaini mapya kwa wakulima hao yalipatikana wiki iliyopita baada ya kupatikana kwa wanunuzi ambao hata hivyo, wamekubali kununua kwa bei ya chini ya wastani wa dola za Marekani 1.25 kwa kilo badala ya bei ya dola mbili kama walivyokuwa wametangaziwa na serikali kabla.

Baadhi ya wakulima waliozungumza na Nipashe walisema kiasi hicho ni kidogo na kamwe hakiwezi kufikia matarajio waliyokuwa nayo.

Hata hivyo, wengi wao walielezea kufarijika kwa kuona kuwa fedha hizo kidogo wanazopata zitasaidia kupunguza machungu ambayo wangeyapata endapo angekosekana kabisa mtu wa kuinunua, hasa kutokana na ukweli kuwa walitumia rasilimali zao nyingi kupata mavuno makubwa msimu huo wa 2016/2017.

Kwa kawaida, tumbaku ikikaa ghalani kwa zaidi ya msimu mmoja hugharimu fedha nyingi kuitunza na pia hushuka ubora wake kabla ya kuharibika na kukosa sifa ya kununuliwa.

 Akizungumza  wakati akiuza sehemu ya tumbaku  iliyokuwa imekosa soko na kubaki ghalani kwa muda mrefu,   Shilinde   alisema wanashukuru kuwa taarifa za kilio chao zimefanyiwa kazi na mamlaka zinazosimamia kilimo cha tumbaku kwa sababu sasa, wameanza kuuza shehena ya zao hilo ijapokuwa ni kwa bei ya chini kulinganisha na matarajio yao.

“Tunashukuru vyombo vya habari ikiwamo Nipashe kwa sababu baada ya habari zenu, kasi ya viongozi wetu huku Kahama kushughulikia tatizo hilo ilionekana kuongezeka. Sasa tunauza tumbaku yetu ingawa ni kwa bei ya chini,” alisema Shilinde.

Aidha, Shilinde alisema pamoja na nafuu ya soko waliyopata, bado anaiomba serikali na mamlaka zilizopewa kusimamia zao hilo kufanya kazi ya ziada kuwatafutia soko la uhakika kwa sababu anaamini kuwa hata baada ya kupatikana kwa wanunuzi wanaowalipa kwa bei ya chini, bado kuna wakulima wengi wataendelea kuwa katika wakati mgumu kwa kushindwa kulipa madeni yote yanayowakabili.

Alisema , akisema kuwa hali hiyo inatishia shughuli za maandalizi ya mashamba ya zao hilo kwa msimu ujao.

Aliongeza kuwa kwa bei wanayouza sasa ya wastani wa  dola 1.25 ni hasara  kwao na kuna baadhi ya  wakulima watashindwa kulipa madeni ya pembejeo  kwenye  vyama  vya msingi  na hilo litaviponza vyama hivyo ambavyo navyo vitashidwa kulipa marejesho ya mikopo kwenye taasisi za fedha.

Alisema kwa kutambua kuwa serikali ya awamu ya tano inajielekeza zaidi katika uchumi wa viwanda, ni vyema mamlaka zenye dhamana ya kusimamia kilimo kikiwamo cha zao la tumbaku waakaongeza juhudi za kutafuta namna ya kuwaimarisha wakulima ili waendelee kuzalisha malighafi za viwanda na siyo kwa mwenendo wa sasa ambao umekuwa ukiwakatisha tamaa, hasa kwa kusikia kuwa wanakosa soko kwa sababu wamezingatia maelekezo ya maofisa ugani katika kulima tumbaku yao na mwishowe kuongeza mavuno maradufu.

 WAKULIMA WANENAAkizungumzia kupatikana kwa wauzaji wa zao hilo, Regina  Ndega , mjane aliyeripotiwa na gazeti hili akieleza alivyoyumba kiuchumi kwa kukosekana wateja, alisema walau sasa amefarijika kuona anapunguziwa hasara kubwa ambayo angeipata kwa kukosekana kabisa wateja. 

Katika kipindi cha kusubiri soko, Ndega alilazimika kujihusisha na biashara ya kuuza maji ili kukabiliana na mahitaji ya kila siku ya familia yake.

Tumbaku yake iliyokosa soko ilikuwa ni kilo 3,000 alizoamini kuwa angepata walau Sh. milioni nane lakini sasa, baada ya kuuza amepata takribani Sh. milioni nne tu.

Alisema hali hiyo imemkatisha tamaa kwa kiasi kikubwa na sasa anafikiria kujihusisha na shghuli nyingine ya ziada na si kumaliza nguvu na mtaji wake wote kwa kulima tumbaku pekee, huku hofu yake ikiwa ni madeni  aliyo nayo dhidi ya malengo yake kiuchumi.

Ndega alisema ni wakati muafaka sasa wa serikali kutupia jicho eneo hilo kwa kuhakikisha kuwa wanaunuzi hawajipangii bei wanayotaka wao kwa sababu mwisho wa siku huwaumiza wakulima.

Naye Zena Magese, alisema anashukuru kuwa tumbaku  yao imenunuliwa, lakini kilichomsikitisha ni ugumu wa soko ambao mwishowe umewafanya walipwe kwa bei ya hasara.

Alisema kutokana na fedha kidogo alizopata, sasa amerudi nyuma kiuchumi hatua nyingi na kibaya zaidi kwake ni kwamba ameshindwa kumudu gharama za  kumpeleka chuo mwanawe na baadhi ya madeni yaliyotokana na maandalizi ya shamba msimu uliopita, hivyo bado hajui ni kwa namna gani atayamaliza.

BODI YA TUMBAKUKwa mjibu wa Kaimu Mkurugenzi  Mkuu wa Bodi ya Tumbaku, Dk.  Julius  Ningu, soko la  tumbaku iliyokuwa  imekosa mnunuzi kwa  nchi nzima , lilipatikana  kupitia mazungumzo ya mara kwa mara  baina  ya serikali na  wanunuzi, ambao ni kampuni za  TLTC na  Allianze One.

Alisema sasa imekubaliwa kuwa tumbaku yote iliyopo kwenye maghala yakiwamo ya Kahama inanunuliwa kwa  wastani huo wa dola za Marekani 1.25.

Ningu alisema kwa mkoa wa kitumbaku wa Kahama, zaidi ya kilo milioni tatu zitanunuliwa na tayari shughuli hiyo imeanza kufanyika.

Dk. Ningu alisema kwa mujibu wa makadirio ya Bodi ya Tumbaku, gharama ya kuzalisha  kilo moja ya zao hilo ni wastani wa zaidi ya  dola  1.25.

Kaimu Mkurugenzi huyo alisema awali walikataa pendekezo la wanunuzi la kulipa bei hiyo ya dola 1.25 lakini wakulima ndiyo waliyoikubali.

Aidha, ofisa anayeshughulikia tumbaku Kahama, Albert  Charles, alikiri kuwa shughuli ya ununuzi wa tumbaku kwenye eneo lake imeanza na baadhi ya wakulima wamefarijika kwa kuona kuwa wanapunguziwa uwezekano wa kupata hasara ya asilimia 100 ya tumbaku ambayo ingebaki kwa kukosa kabisa mnunuzi.

 MKUU WA MKOA

Akizungumzia kilio cha soko kwa wakulima wa tumbaku, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainabu Tellac, alisema suala hilo lilikuwa likishughulikiwa na Wizara ya Kilimo na kwamba sasa, mkakati walionao mkoani kwake ni kuhakikisha kuwa linapatikana soko la uhakika kwa zao hilo.

Alisema tayari walishafanya vikao na wakulima wa tumbaku na wadau mbalimbali wa zao hilo na kwamba sasa wako kwenye mazungumzo ya pamoja  kuona kuwa wanaanzisha kiwanda cha sigara  pamoja na kutangaza  fursa  kwa wawekezaji  ili kusaidia kupatikana kwa soko la uhakika la tumbaku  na kuondokana na urasimu uliopo sasa katika soko la zao hilo.

Aidha, wawakilishi wa kampuni za TLTC na Alliance  One  walioko Kahama walipotakiwa kuzungumzia suala hilo, kwa nyakati tofauti walisema jambo hilo lilikuwa  linashughulikiwa na ngazi ya wizara na hivyo hawawezi kulizungumzia . 

Habari Kubwa