Prof. Maghembe awapa angalizo wabunge CCM

18Jul 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Prof. Maghembe awapa angalizo wabunge CCM

MBUNGE wa Mwanga mkoani Kilimanjaro kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Prof. Jumanne Maghembe, amesema wabunge waepuke kupanga safu katika uongozi wa chama ngazi ya jimbo ili kuepuka kukidhoofisha chama.

Prof. Jumanne Maghembe

Prof. Maghembe ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii, alisema hayo hivi karibuni akiwa katika ziara jimboni kwake kukagua ni kwa kiwango gani ilani ya CCM inatekelezwa hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi wa ndani.
 
“Kwenye jimbo langu uchaguzi unakwenda vizuri, huwa nahamasisha uhai wa chama kwa ujumla ndio maana utaona nilichangia fedha za kuimarisha majengo ya tawi,” alisema na kuongeza: “Nikiwa mbunge naepuka kujenga safu yaani kutafuta watu wangu.
 
“Nahamasisha watu wote wawe na fursa za kuchagua na kuchaguliwa, watakaopatikana ndio tunaunda safu kuimarisha chama. Kwa sababu hiyo ndiyo maana katika Mkoa wa Kilimanjaro hapa Mwanga chama kipo imara kwa sababu mbunge wala viongozi wengine wa juu hawana makundi.”
 
Akizungumza kwa nyakati tofauti kwenye ziara hiyo ya jimbo, Prof. Maghembe alisema wamejiwekea malengo ya kutekeleza ilani ya chama kwa miaka mitano na kuainisha vipaumbele vya kuanza navyo.
 
Akizungumzia umuhimu wa elimu waziri huyo ambaye aliwahi kupewa dhamana ya kusimamia Wizara ya Elimu katika serikali ya awamu iliyopita alisema: “Katika jimbo hili tumepiga hatua na sasa tunapeleka watoto 4,200 kujiunga na  sekondari kutoka watoto 300 hapo awali, pia tuna uhakika wa kuwa katika shule kumi bora zenye ufaulu mzuri kitaifa.
 
“Kipaumbele cha pili ni afya, kwa sasa Wilaya ya Mwanga ina vijiji 72 na malengo ni kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na zahanati. Mpaka sasa tumejenga zahanati 54 na zingine zinaendelea kujengwa.”
 
Mbali na vituo vya afya, lakini pia alibainisha mpango wa kujenga hospitali kubwa eneo la Mwanga wilayani, kutokana na ongezeko la watu katika eneo hilo kutokana na kupita barabara kubwa.
 
Aidha, kutokana na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Magufuli kuazimia kuwa na uchumi wa viwanda Prof. Maghembe alisema wilayani kwake kuna kiwanda kimoja kikubwa ambacho kimeajiri watu zaidi ya 130 na mapato yake ni Dola za Kimarekani milioni 4 kwa mwaka, zaidi ya Sh. bilioni 8.
 
“Mbali ya kiwanda hicho, vipo viwanda vingine vidogovidogo hii ni kutokana na idadi kubwa ya wakazi wa Mwanga kuwa wakulima na wafanyabiashara,” alisema.
 
CCM iko katika mchakato wa uchaguzi wa ndani kuanzia ngazi ya shina, kata, wilaya, mkoa hadi taifa ili kupata viongozi.

 

Habari Kubwa