Polisi yasema itamshughulikia Adbul Nondo

08Mar 2018
Gerald Kitalima
Nipashe
Polisi yasema itamshughulikia Adbul Nondo

Jeshi la Polisi Mkoani Iringa limefunguka na kuweka wazi kuwa mwanafunzi wa mwaka wa tatu UDSM, Adbul Nondo alifika kituo hicho cha polisi jana Machi 7, 2018 na kusema kuwa alitekwa na watu wasiojulikana. 

Kwa mujibu wa RPC wa mkoa huo, Juma Bwire, amesema jeshi la polisi limefungua jalada la uchunguzi ili kubaini ukweli kama mwanafunzi huo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania kama kweli alitekwa au la.

"Jeshi la polisi mkoa wa Iringa limefungua jalada la uchunguzi kubaini ukweli kama alikuwa ametekwa na kama alitekwa tunaahidi kwamba sisi jeshi la polisi likiwapata watuhumiwa sheria itachukua mkondo wake aidha tunaendelea kuchunguza kama ametoa taarifa za uongo kwa njia ovu kwa lengo la kutaka kuhamasisha wanafunzi wenzake ili kuleta uvunjifu wa amani nchini tutamshughulikia kama waalifu wengine" 

Aidha RPC amesema kuwa mwanafunzi huyo kwa sasa anaendelea vizuri na wala hana majeraha yoyote yale kwani hajapigwa na ni mzima wa afya njema na kusema jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kujua nini kilimsibu. 

Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania Abdul Nondo alipotea katika mazingira ya kutatanisha Machi 6, 2018 akiwa jijini Dar es Salaam majira ya saa tano usiku na kupatikana Mafinga Iringa Machi 7, 2018.   

Habari Kubwa