NSSF yakomboa bil. 90/-

21Apr 2017
Salome Kitomari
Nipashe
NSSF yakomboa bil. 90/-

SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), limekusanya Sh. bilioni 90 kutoka kwa wadaiwa sugu na fedha hizo sasa zimeelekezwa kwenye kutekeleza miradi ya maendeleo, ikiwamo uwekezaji kwenye viwanda.

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara.

Akizungumza na Nipashe katika mahojiano maalum, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara alisema baadhi wadaiwa sugu wamefikishwa mahakamani kwa kushindwa kutimiza wajibu wa kisheria.

Alisema makusanyo hayo yametokana na waajiri mbalimbali ambao kwa muda mrefu hawakuwa wamelipa michango ya wanachama ambayo ipo kisheria.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, waajiri waliokuwa wakidaiwa kiasi hicho ni idara za serikali, mashirika ya umma na sekta binafsi na kwamba ambao hawajamaliza madeni yao wameingia makubaliano maalum ya kulipa kwa wakati.

“Kwa sasa NSSF haina wadaiwa sugu," alisema Prof Kahyarara. "Tuna waajiri zaidi ya 25,000 wanaoleta michango yao, (na) kutokana na kulipa kwa wakati tumeongeza makusanyo kutoka Sh. bilioni 45 hadi Sh. bilioni 65 kwa mwezi.”

Aidha, Prof Kahyarara alisema kuna kesi 250 katika mikoa mbalimbali nchini dhidi ya waajiri ambao wameshindwa kupeleka michango, idadi ambayo alisema ni kidogo sana, hata hivyo, ikilinganishwa na waajiri ambao wana wanachama wa NSSF.

“Haya yote yamefanikiwa kwa kuwa tumeimarisha kitengo cha ulinzi cha Shirika ambacho kina wapelelezi wa ngazi ya RCO ambacho hakikuwa kinatumika kabisa," alisema.

"Tunawapa fedha na ndiyo wanafanya uchunguzi ambao unasaidia kuokoa mabilioni ya fedha yanayoelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.”

Alisema kwa sasa kuna ufuatiliaji kwa karibu kuhakikisa madeni yote ya shirika yanalipwa na wanaoshindwa kutekeleza mkondo wa sheria utachukua hatua dhidi yao.

“Ukusanyaji wa madeni kama haya unatupa nguvu zaidi kuwekeza kwenye miradi mikubwa ya maendeleo ikiwamo viwanda.”

Alisema pamoja na mafanikio hayo, NSSF imebana matumizi kwa asilimia 30 na kuwezesha kupatikana kwa fedha zaidi za kuelekeza kwenye uwekezaji ambao hautavuka kiwango kilichowekwa kisheria.

Alisema kwa mujibu wa sheria, mifuko ya hifadhi ya jamii haitakiwi kukusanya fedha na kukaa nazo bali kuziwekeza ili ziongeze thamani.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, NSSF imesitisha uwekezaji kwenye majengo ambao ulishavuka kiwango kilichowekwa kisheria na sasa wameelekeza nguvu kwenye viwanda ambako hakukukua na uwekezaji wowote.

NSSF itatengeneza zaidi ya ajira 100,000 baada ya kukamilika kwa mchakato wa kushiriki katika uchumi kwa viwanda.

Ajira hizo zitatokana na viwanda vya sukari vya Mbigili na Mkulazi, kiwanda cha Viuadudu cha Kibaha, viwanda vya nafaka vya Iringa na Dodoma na kiwanda cha chaki mkoani Simiyu.

Mbali na kuzalisha ajira hizo, Prof Kahyarara alisema uwekezaji huo pia utaliwezesha shirika kupata wanachama zaidi ambao watachangia katika mfuko, kuboresha huduma za jamii na kuleta maendeleo kwa ujumla.

Habari Kubwa