NEC yatangaza tarehe ya uchaguzi

03Jan 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
NEC yatangaza tarehe ya uchaguzi

Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini (NEC) imesema uchaguzi mdogo katika majimbo ya Siha - Kilimanjaro, Kinondoni mkoani Dar es Salaam na Kata nne za Tanzania Bara utafanyika Feb 17, 2018 kufutia waliokuwa wabunge katika majimbo hayo kujivua uanachama.

Makamu Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mkuu Mstaafu wa Zanzibar, Hamid Mahmod Hamid.

Taarifa ya Makamu Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mkuu Mstaafu wa Zanzibar, Hamid Mahmod Hamid, imeeleza kuwa pamoja na majimbo hayo, pia Kata nne za Isamilo , Manzase, Madanga ndizo zitafanya Uchaguzi mdogo

Aidha, Jaji Hamid amesema, Tume inaendesha uchaguzi huo baada ya kupokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai kuhusu kuwepo wazi kwa jimbo la Kinondoni jijini Dar es Salaam na jimbo la Siha mkoani Kilimanjaro.

Amesema, barua hiyo ilieleza kuwa majimbo hayo yapo wazi baada Maulid Mtulia aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kinondoni kujivua uanachama wa CUF na Dk. Godwin Mollel wa jimbo la Siha kujiuzulu uanachama wa CHADEMA na hivyo wote kukosa sifa za kuendelea kuwa wabunge.

Pia, ameeleza kuwa Tume ilipokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa ikiitaarifu Tume uwepo wa nafasi wazi za Udiwani katika kata nne za Tanzania Bara.

Hivi karibuni kumekuwa na wimbi la viongozi kuhama vyama vyao vya siasa na kuhamia vyama vingine hali ambayo serikali inalazimika kuandaa chaguzi nyingine ili kujaza nafasi zinazoachwa wazi. Uchaguzi wa mwisho wa marudio ulifanyika Nov 26, 2017 huku mwingine ukitarajiwa kufanyika Januari 13 mwaka huu.

 

Habari Kubwa