Ndama akiri kutakatisha Dola 540,000

19May 2017
Hellen Mwango
Nipashe
Ndama akiri kutakatisha Dola 540,000

MFANYABIASHARA Ndama Shabani Hussein maarufu kama Ndama Mtoto ya Ng’ombe, amekiri mahakamani kutakatisha Dola za Kimarekani 540,000 (sawa na zaidi ya Sh. bilioni 1.2 kwa kiwango cha kubadilishia cha jana).

Ndama Mtoto ya Ng’ombe.

Ndama alikiri shtaka la kutakatisha fedha kati ya mashtaka sita yanayomkabili katika kesi hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Kisutu, Victoria Nonga.

Mapema jana, Wakili wa Serikali, Esterzia Wilson, alidai kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa maelezo ya awali ya mshtakiwa huyo jana baada ya kukiri kosa la kutakatisha fedha.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo alikana shtaka la kwanza hadi la tano ambayo upelelezi wake haujakamilika.

Kutokana na upande wa Jamhuri kutokuwa na jalada halisi la kesi hiyo, hakimu Nongwa alisema mshtakiwa atasomewa maelezo yake ya awali Jumatano.
Kwa mujibu wa Sheria ya Kutakatisha Fedha, Ndama anaweza kuhukumiwa kifungo cha miaka isiyopungua mitano hadi 10 au kulipa faini kati ya Sh. milioni 100-Sh. milioni 500.

Katika shtaka alilolikubali Ndama, la sita, anadaiwa kati ya Februari 26 na Machi 2014, Dar es Salaam, akiwa mwenyekiti na mtia saini pekee wa kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Limited na akaunti ya benki ya kampuni hiyo iliyoko kwenye benki ya Stanbic, alijihusisha moja kwa moja kwenye uhamishaji wa dola za Marekani 540,000 na kuzitoa huku akijua fedha hizo sio halali na ni kosa la uhalifu la kujiapatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Ndama pia anadaiwa Februari 20, 2014 Dar es Salaam, alighushi nyaraka ya kibali cha kusafirisha madini na sampuli za madini kwa kusudi la kuonyesha kuwa kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited iliruhusiwa kusafirisha makasha manne ya dhahabu yenye kilo 207 yenye thamani ya Dola za Marekani 8,280,000.00 kwenda Australia kwa kampuni ya Trade TJL DTYL Limited wakati akijua si kweli.

Pia anadaiwa Machi 6, 2014, Dar es Salaam, alighushi kwa kutengeneza hati ya kibali ya Umoja wa Mataifa ofisi ya Dar es Salaam akijaribu kuonyesha kilo 207 za dhahabu kutoka Congo zinatarajiwa kusafirishwa na kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited kwenda Australia kwa kampuni ya Trade TJL DTYL Limited, zimesafirishwa bila jinai yoyote wakati akijua si kweli.

Aidha, Ndama anadaiwa Februari 20, 2014, alighushi fomu ya forodha yenye namba za usajili R.28092 akionyesha kampuni ya Muru imeilipa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) dola za Marekani 331,200 kama kodi ya uingizaji wa bidhaa ambazo zina uzito wa kilo 207 za dhahabu zenye thamani ya Dola za Marekani 8,280,000 kutoka Congo.

Katika shtaka lingine anadaiwa Februari 20, 2014, alighushi nyaraka ya bima kutoka Phoenix of Tanzania Assurance Company Ltd akionyesha kampuni ya Muru imeyawekea bima makasha manne yaliyokuwa na dhahabu hizo.

Anadaiwa kati ya Februari 26 na Machi 3, 2014, Dar es Salaam kwa njia ya udanganyifu alijipatia kutoka kwa kampuni ya Trade TJL DTYL Limited ya Australia Dola za Marekani 540,000 baada ya kudanganya ataipa na kusafirisha dhahabu hizo.

Habari Kubwa