Nape ashangaa ukimya sakata kutolewa bastola

09Apr 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Nape ashangaa ukimya sakata kutolewa bastola

ALIYEKUWA Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, ameelezea kushangazwa kwake na ukimya wa Jeshi la Polisi kuhusiana na mtu aliyemtolea bastola hadharani hivi karibuni.

mbunge wa Mtama mkoani Lindi, Nape Nnauye.

Nape alieleza hayo jimboni kwake Mtama mkoani Lindi jana wakati akiwahutubia wapiga kura wake kwa mara ya kwanza tangu alipoondolewa katika nafasi ya uwaziri.

Akizungumza kwenye mkutano huo ambao ulitanguliwa na tukio la yeye kupita juu ya miili ya kina mama waliojitokeza kumlaki mkutanoni ikiwa ni sehemu ya utamaduni wao kwa viongozi, Nape alisema inashangaza kuona hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi ya mtu huyo aliyemtolea bastola katika siku aliyozungumza na waandishi wa habari kuelezea msimamo wake baada ya kuondolewa katika uwaziri.

“Shida niliyonayo huyu jambazi aliyetoa silaha, vyombo vya ulinzi na usalama vinafanya naye nini...kama wameweza kumfanyia Nape, Watanzania wangapi watafanyiwa huku mitaani?’ alihoji Nape, akisistiza kuwa kitendo hicho hakikuwa cha kiungwana na mhusika alipaswa kuchukuliwa hatua.

Nape aliondolewa uwaziri na nafasi yake kutwaliwa na Dk. Harrison Mwakyembe baada ya kupokea ripoti ya Kamati aliyoiunda kuchunguza tukio la uvamizi wa kituo cha televisheni na radio cha Clouds, uliodaiwa kufanikishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Awali, Mwakyembe alikuwa akiongoza Wizara ya Sheria na Katiba.

Hadi sasa, ikiwa ni zaidi ya wiki mbili tangu Nape atolewe bastola hadharani, haijaelezwa kama mhusika amepatikana licha ya kuwapo kwa agizo lililotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba kuwa mtu huyo asakwe na kuchukuliwa hatua.

ATOA AHADI
Katika mkutano wake wa jana, Nape aliahidi kuwa atatumia nguvu na uwezo wake wote kuhakikisha jimbo la Mtama linakuwa na maisha bora.

Akizungumzia kuondolewa uwaziri, Nape alisema yalikuwa ni mabadiliko ya kawaida na uthibitisho ni taarifa iliyotolewa na Ikulu kuhusiana na mabadiliko hayo.

Habari Kubwa