Mwigulu afichua mapya miili baharini

03Jan 2018
Mary Geofrey
Nipashe
Mwigulu afichua mapya miili baharini

WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema miili ya watu iliyookotwa katika fukwe za bahari na maeneo mbalimbali nchini katika kipindi cha mwaka jana, ilikuwa ya wahamiaji haramu.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Dk. Mwigulu Nchemba.

Amesema wahamiaji hao walikuwa wakisafirishwa kutoka nje ya nchi kwa kutumia magari ya mizigo ambayo hayana hewa hali iliyosababisha kupoteza maisha na kutupwa.

Mwigulu alifichua hayo jana mkoani Dodoma, wakati akizungumza kuhusu malengo ya wizara hiyo, katika mwaka 2018 na changamoto za mwaka 2017.

“Watu waliokuwa wakiwabeba wakifika sehemu wakikuta wamepoteza maisha kwa sababu ya kukosa hewa na chakula wanaamua kuwatupa sehemu mbalimbali, maeneo mengine tuliwaokota wahamiaji wakiwa hoi,” alisema.

Dk. Nchemba alisema kwa mwaka huu wamejipanga kukabiliana na matukio hayo kwa kuweka sheria kazi za kudhibiti wanaowabeba na kwamba watakaokamatwa watachukuliwa hatua kali za kisheria na chombo kitakachokamatwa kitataifishwa.

Kuhusu tukio lililomshtua na kumuhuzunisha mwaka 2017, alisema ni lile la kupokea kwa watu, kushambuliwa viongozi wa vijiji na askari polisi maeneo Kibiti, mkoani Pwani.

“Kwa mwaka 2017 matukio yaliyoniudhi zaidi ni tukio la kushambuliwa kwa askari polisi na wananchi katika maeneo ya Kibiti… kushambuliwa kwa kiongozi mchana tena katikati ya mji wa serikali na watu kupotea sehemu kusiko julikana,” alisema Dk. Nchemba.

Aliwataka wananchi kuwa mstari wa mbele kuripoti na kuibua matukio yanayopangwa kufanyika, ili Jeshi la Polisi liweze kudhibiti mapema.Kadhalika, Dk. Nchemba alisema mwaka huu, wizara hiyo inalengo la kukaa na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kupanga namna ya kuweka utaratibu wa adhabu ikiwezekana ya kufanya kazi kwa wale wenye makosa madogo.

Alisema kwa wale walioshindwa kulipa fedha baada ya kufanya makosa madogo madogo, ili kupunguza msongamano wa mahabusu magerezani.

“Kwa kuwaweka zaidi magerezani ni kuwachanganya na wafungwa wazoefu na wanaweza kufundishwa kufanya makosa zaidi,” alieleza. 

Habari Kubwa