Mwakalebela aibukia ubunge Afrika Mashariki

20Mar 2017
Ibrahim Joseph
Nipashe
Mwakalebela aibukia ubunge Afrika Mashariki

MAKADA 18 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamejitokeza kuchukua fomu za kugombea ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kupitia Chama hicho huku kukiwa na idadi kubwa ya vijana.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Fredrick Mwakalebela.

Miongoni mwa walijitosa kuwania nafasi hiyo ni pamoja na aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Fredrick Mwakalebela.

Mwakalebela aligombea ubunge katika jimbo la Iringa Mjini katika uchaguzi wa 2015, lakini aliangushwa na Mchungaji Peter Msigwa (Chadema).

Wanachama hao walijitokeza jana ikiwa ni siku ya kwanza ya kuanza kutolewa kwa fomu hizo katika Ofisi za Makao Makuu ya chama hicho mjini Dodoma.

Nipashe ilishuhudia makada hao wakimiminika kuchukua fomu saa 2 asubuhi na hadi saa 8 mchana. Makada hao walikabidhiwa fomu na Ofisa wa Idara ya Organaizesheni, Jackson Shalua.

Wengine aliochukua fomu hizo ni Hamisi Malinga (Dodoma), Janeth Marwa, Erick Kato, Victory Mollel, Julius Mungure na mwalimu Lorinyu Mkoosi, wote kutoka mkoa wa Arusha.

Wengine ni Dk. Augustino Mwakipesile, Rehema Mrosso, Richard Mbilinyi, Senorina Munubi na Daniel Illakwahhi (Manyara).

Wamo pia Kisanko Evance na Asanjile Mwambambale kutoka mkoa wa Mbeya. Kwa mkoa wa Singida ni Dk. Pius Chaya na Martin Lissu.

Aliyejitokeza kutoka mkoa wa Dodoma ni Emanuel Kamara na mkoa wa Mwanza ni Sitta Ngissa.

Akizungumza na Nopashe, Mwalimu Lorinyu Mkoosi alisema amejitokeza kama kijana ili kuliwakilisha Taifa katika bunge hilo na kwamba Taifa lolote bila vijana haliwezi kuendelea kwa sababu vijana wana nguvu, ni wachapa kazi na wana mtazamo wa kasi zaidi.

“Mimi unavyoniona niligombea ubunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi wa 2015 na nilishika nafasi ya tatu, lakini sikati tamaa kwa sababu ni lengo la kuwaletea maendeleo wananchi wenzangu na sasa nimechukua fomu hizi,” alisema Mkoosi.

Aidha, alisema kutokana na uwezo wake anaona anazo sifa za kupitishwa kugombea nafasi hiyo.

Taarifa iliyotolewa juzi na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, ilieleza kuwa chama hicho kingeanza kutoa fomu hizo kuanzia jana hadi Machi 23.

Alivitaja vituo vya kuchukulia fomu kuwa ni Makao Makuu Dodoma, Ofisi Kuu ya Makao Makuu Zanzibar na Ofisi ndogo ya Makao makuu Dar es Salaam katika Idara ya Organaizesheni kwa malipo ya Sh. 100,000.

Polepole alisisitiza katika uhalisia wa mageuzi makubwa ya CCM ambayo yanalenga kuwapatia aina ya viongozi waadilifu, waaminifu, wachapakazi, wawajibikaji na wanaochukizwa na rushwa.

Alisema waomba ridhaa watakaoonyesha mwenendo na vitendo kukiuka Katiba ya CCM, kanuni za uchaguzi za CCM na kanuni za uongozi na maadili za CCM, uongozi na vikao vya chama havitakuwa na ajizi kuwachukulia hatua ikiwa ni pamoja na kuwaondolea sifa ya uteuzi.

Habari Kubwa