Muswada kuunganisha mifuko  hifadhi jamii wasomwa bungeni 

18Nov 2017
Sanula Athanas
Nipashe
Muswada kuunganisha mifuko  hifadhi jamii wasomwa bungeni 

MUSWADA wa Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma wa mwaka 2017 ulisomwa kwa mara ya kwanza bungeni jana, ukilenga kuunda sheria itakayoiunganisha mifuko hiyo ili ibaki miwili.

Muswada huo ulisomwa bungeni mjini hapa mara tu baada ya kumalizika kwa kipindi cha 'Maswali', huku mifuko ya GEPF, LAPF na PPF ikitajwa wakati wa kusomwa kwake.

Mifuko mingine ya hifadhi ya jamii iliyopo nchini ni PSPF na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) ambalo linashughulika na sekta binafsi.

Kuwasilishwa kwa muswada huo kumefanyika ikiwa ni siku mbili baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, kukiahidi chombo hicho cha kutunga sheria kwamba serikali itawasilisha bungeni muswada wa kuiunganisha mifuko ya hifadhi ya jamii.

Akijibu hoja iliyoibuliwa na Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea (CUF) wakati wa mjadala wa Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 4 wa mwaka 2017 bungeni mjini hapa Jumatano, AG Masaju alisema muswada wa kuiunganisha mifuko ya hifadhi ya jamii nchini ulitarajiwa kusomwa bungeni kwenye mkutano wa tisa uliomalizika jana.

Katika hoja yake siku hiyo, Mtolea mwenye shahada ya sheria, alihoji sababu za serikali kutowasilisha bungeni muswada utakaounganisha mifuko hiyo badala yake iliwasilisha marekebisho kuhusu Mfuko wa Mfumo wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ambao alidai ni sehemu ya mifuko ya hifadhi ya jamii.

Mbunge huyo alisema Rais John Magufuli amekuwa akieleza kuhusu kusudio la kuiunganisha mifuko hiyo kuwa na miwili itakayohudumia wafanyakazi kutoka serikali na sekta binafsi.

Hata hivyo, AG Masaju alimtaka mbunge huyo kutofautisha kati ya Sheria ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi na Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa kuwa vitu viwili tofauti na ndipo akatoa ahadi ya kuwasilisha muswada wa sheria ya itakayoiunganisha mifuko hiyo kwenye mkutano huo wa bunge uliohitimishwa jana.

Muswada mwingine uliosomwa kwa mara ya kwanza jana ni wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 5) wa mwaka 2017.
Katika kikao cha jana cha bunge, Muswada Marekebisho ya Sheria ya Hifadhi ya Wanyamapori ya mwaka 2017 ulisomwa kwa mara ya pili.

Habari Kubwa