Muhimbili yajitosa kumtibu ‘mama wa jicho’ bure mwenye tatizo la jicho

28Dec 2017
Peter Mkwavila
Nipashe
Muhimbili yajitosa kumtibu ‘mama wa jicho’ bure mwenye tatizo la jicho

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) imejitolea kutoa matibabu ya upasuaji wa jicho kwa Adda Juma (40) mkazi wa Mtera wilayani Mpwapwa, Dodoma bila malipo.

Uamuzi wa hospitali hiyo umechukuliwa siku moja baada ya Nipashe katika toleo lake la jana kuchapisha habari akiomba msaada wa Sh. milioni tano kwa ajili ya matibabu katika Hospitali ya Muhimbili.

Kwa mujibu wa habari hizo, Adda amekuwa akisumbuliwa na tatizo hilo kwa miaka mitatu sasa na amekwenda katika hospitali kadhaa ikiwamo ya Mvumi Misheni, Dodoma bila mafanikio. 

Adda alisema tatizo hilo ambalo lilianza toka mwaka 2015 limemtesa na kusababisha shughuli zote za kujitafutia kipato kusimama na hatimaye kujikuta akiwa maskini huku akitegemea misaada kutoka kwa watu. 

Kutokana na taarifa hiyo, Msemaji wa MNH, Aminiel Aligaesha, alipiga simu Nipashe jana asubuhi na kuiarifu kuwa hospitali hiyo kubwa zaidi nchini, iko tayari kutoa huduma za matibabu kwa mgonjwa huyo bila malipo.

"Tumesoma gazeti lenu asubuhi hii na kuguswa sana na habari iliyoko ukurasa wa nne ya mama anayeomba msaada wa kutibiwa jicho," Aligaeshi alisema na kuongeza:

"Kwa kuwa sisi (MNH) hatuna mawasiliano na huyo mama, tunaomba mmwaarifu kwamba Muhimbili tuko tayari kumtibu bila malipo yoyote. Aje tu, madaktari wetu wanamsubiri kumhudumia."

Akizungumza na Nipashe jana kwa njia ya simu, mama mzazi wa Adda, Anna Fungameza, alishukuru uongozi wa Hospitali ya Muhimbili kwa msaada huo.

Pia alishukuru gazeti la Nipashe kwa kuchapisha habari kuhusu ugonjwa wa mwanawe akiamini kuwa sasa mtoto wake ataondokana na tatizo la jicho lililomtesa kwa miaka mitatu.

“Ninashukuru kwa Nipashe kunitembelea na kuniandikia habari za tatizo la mwanangu ambaye kwa miaka yote hiyo nilikuwa nimekata tamaa ya kupona. Pia ninashukuru uongozi wa Muhimbili kwa kukubali kumtibu mwanangu bure,” alisema.

Habari Kubwa