Mshtuko Dar

23Nov 2017
Na Waandishi Wetu
Nipashe
Mshtuko Dar

NI Mshtuko! Imebainika kuwa wakazi wengi wa jiji la Dar es Salaam wako hatarini kiafya kutokana na kukabiliwa na maradhi ya moyo, shinikizo la damu maarufu kama presha, uoni hafifu na kisukari.

Ukweli huo wa kushtua unatokana na matokeo ya vipimo vilivyofanyika hadi sasa kwa mamia ya wakazi wa jiji hilo kupitia zaidi ya madaktari 300 waliomo kwenye meli ya Kichina ya Ark of Peace, iliyoko kwenye Bandari ya Dar es Salaam tangu juzi kwa ajili ya kutoa huduma bure za matibabu.

Magonjwa mengine yaliyobainika kwa kiasi kidogo miongoni mwa wale waliohudumiwa hadi kufikia jana ni matatizo ya mgongo, saratani za aina mbalimbali na kuvimba miguu.

Aidha, imefahamika kuwa miongoni mwa sababu za kuwapo kwa watu wengi wenye maradhi hayo jijini Dar es Salaam ni pamoja na uvivu wa baadhi ya watu ambao huwa hawajihusishi na mazoezi ya mwili hata mara moja kwa mwezi; baadhi yao kutoupa mwili nafasi ya kuchangamka kwa kutembea kwa miguu kutokana na uwapo wa usafiri wa kutosha wa vyombo vya moto kama bodaboda na bajaji; unywaji kupita kiasi wa bia na ulaji usiozingatia mpangilio wa mlo kamili na badala yake wengi wao kuendekeza nyama choma, chipsi mayai na wanga uliopitiliza kupitia ugali na wali karibu kila uchao.

Zaidi ya madaktari bingwa 300 wa Kichina ndio wanaotoa huduma hizo kwa mamia ya wananchi wanaofika kwenye meli hiyo tangu siku ya kwanza.

Kuanzia jana, madaktari wengine kutoka katika Hospitali za Muhimbili, Ocean Road, Temeke, Amana, Mwananyamala, Taasisi ya Mifupa (MOI) na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) waliongezwa kwenye meli hiyo kwa ajili ya kukabiliana na mahitaji makubwa ya huduma kutokana na umati unaojitokeza kila uchao.

Meli hiyo iliyoanza kutoa huduma Jumatatu baada ya kutua nchini kutokana na jitihada za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kwa ajili ya watu wa mkoa wake, inatarajiwa kukamilisha kazi hiyo keshokutwa.

Desemba, mwaka jana, Makamu wa Rais, Samia Suluhu, aliitangaza kila Jumamosi ya pili ya mwezi kuwa maalumu kwa ajili ya watu wote kufanya mazoezi nchini, ili kupunguza uwezekano wa kupatwa na maradhi yanayoepukika kirahisi, yakiwamo ya kisukari na presha.

MGANGA MKUU DAR

Akitoa taarifa jana kuhusiana na huduma za afya zinazotolewa ndani ya meli hiyo kuanzia Jumatatu, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Grace Maghembe, alisema watu 650 walihudumiwa juzi, idadi ambayo ni kubwa zaidi ya matarajio ya kuhudumia wastani wa wagonjwa 600 kwa siku.

"Kwa siku ya jana (juzi), wananchi 650 walipata matibabu na idadi kubwa ya waliopimwa wanasumbuliwa na maradhi haya haya ya siku zote… presha,  kisukari,  macho, na moyo,” alisema Dk. Maghembe na kuongeza:

“Wachache sana wamegundulika kuwa na matatizo ya mgongo, saratani na miguu kuvimba. " Dk. Maghembe alisema idadi ya wananchi wanaojitokeza kupata matibabu katika meli hiyo ni kubwa kuliko ilivyodhaniwa ndipo serikali ya mkoa wa Dar es Salaam ilipolazimika kuongeza madaktari bingwa kutoka hospitali zilizoko jijini Dar es Salaam ambao watakuwa wanawatibia wagonjwa kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni.

"Kesho (leo) madaktari hao wataanza kutoa huduma,  wengine watakuwa eneo la bandarini,  wengine watakuwa eneo la kituo kikuu cha polisi,  na watatoka hospitali za Mwananyamala,  Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH),  Taasisi ya Saratani ya Ocean Road,  Amana,  Mwananyamala,  Taasisi ya Mifupa Moi na wengine wameanza leo (jana), " alisema Dk. Maghembe. Alisema madaktari hao watakuwa wakitoa huduma muda wote kwa sababu madaktari kutoka China ifikapo mchana huwa wanapumzika.

Alisema hadi kufikia Jumamosi, kazi ya kutoa matibabu itakuwa imemalizika na kwamba anaamini kuwa madaktari kutoka China watakapoondoka, wananchi wote watakaofika watakuwa wameshapatiwa matibabu.

Aidha, Dk.  Maghembe alisema katika meli hiyo, baadhi ya huduma zinazotolewa ni pamoja na upasuaji mdogo na matibabu mengine madogo, lakini akisisitiza kuwa hawafanyi upasuaji mkubwa kama baadhi ya watu wanavyodhani.

Alisema endapo mgonjwa akikutwa na tatizo kubwa linalohitaji upasuaji mkubwa, anakabidhiwa kwa madaktari wa Muhimbili ambao ndiyo watashughulikia tatizo lake katika hospitali za hapa nchini.

Jana, mwandishi wa Nipashe alishuhudia foleni ndefu ya watu waliofika kupata huduma ikiwa katika eneo la Kituo Kikuu cha Polisi ambako wahusika walikuwa wakisubiri kupata namba pamoja na kupelekwa katika eneo la bandari ilikotia nanga meli hiyo kwa ajili ya huduma.

Katika eneo la bandari ambako meli hiyo imetia nanga, mwandishi alishuhudia idadi kubwa ya wananchi waliokuwa kwenye foleni wakisubiri kupatiwa huduma huku baadhi yao wakikiri kukata tamaa kwa kujiona wako nyuma zaidi kwenye foleni na kuamua kuondoka.

Kwa mujibu wa waratibu, meli hiyo yenye urefu wa mita 178, ina vifaa tiba pamoja na vyumba nane vya upasuaji, vyumba vya wagonjwa mahututi (ICU), wodi za wagonjwa, vyumba vya madaktari, mitambo ya kisasa, maabara na sehemu ya kupumzikia wagonjwa.

CHANZO DAR KUSHAMIRI KISUKARI, PRESHA

Wakizungumza na Nipashe jana, baadhi ya madaktari walisema kuwa kushamiri kwa maradhi ya moyo, presha, kisukari na uoni hafifu huchangiwa kwa kiasi kikubwa na aina ya maisha ya wakazi wengi wa jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine ya miji nchini.

Ulaji wa vyakula usiozingatia mlo kamili, uvivu wa mazoezi, kutofanya kazi za kutosha zitoazo jasho mwilini na utumiaji wa vyombo vya moto vya usafiri kama magari na bodaboda hata kwa umbali mfupi mijini ni miongoni mwa sababu za kushamiri kwa magonjwa hayo.

Kuhusu chanzo cha kushamiri maradhi hayo, Dk. Baldwin Kileo wa Hospitali ya Rabininsia Memorial ya Tegeta jijini Dar es Salaam, alisema sababu kubwa ni moja tu ambayo ni aina ya maisha ya watu wengi wa mijini. “Kisababishi kikuu cha kisukari na presha au moyo ni aina ya vyakula tunavyokula.

Tumeacha vyakula vya asili, tunakula mafuta yasiyo rafiki… mafuta mazuri ni yale yatokanayo na mimea,” alisema. Aidha, alisema mbali na vyakula hivyo, wananchi wengi hawafanyi mazoezi na hutumia muda mwingi kwenye magari au kukaa kwenye viti ofisini.

Aliyataja makundi ambayo yako kwenye hatari kubwa ya kupata kisukari kuwa ni wale wenye uzito mkubwa, wenye historia ya magonjwa ya kisukari katika familia zao, watu wasiojishughulisha au wasiofanya mazoezi, wenye shinikizo la damu, msongo wa mawazo na wenye matumizi makubwa ya sigara na pombe.

Daktari wa Magonjwa ya Binadamu na mtaalamu wa masuala ya lishe, Boaz Mkumbo, alisema magonjwa yanayowasumbua wakazi wengi mijini chanzo chake ni lishe duni na mifumo ya maisha, ikiwamo unywaji wa pombe kupita kiasi pasi na kujihusisha na mazoezi.

“Visingizio vya watu wengi ni kwamba tumerithi, ila haya ni magonjwa ya kileo kwa sababu huko nyuma hayakuwapo kwa kiwango hiki (kikubwa) cha sasa,” alisema.

Alisema kuna haja sasa kwa serikali na wadau wa masuala ya afya na lishe kutoa elimu ya kutosha kuhusu lishe bora.  “Elimu ya lishe imeelekezwa zaidi kwenye tiba baada ya mtu kuugua… ulaji wa vyakula vya sukari na wanga ni miongoni sababu na pia watu hawafanyi mazoezi,” alisema Dk. Mkumbo.

Habari Kubwa