Miti milioni moja Mlima Kilimanjaro

03Jan 2018
Mary Geofrey
Nipashe
Miti milioni moja Mlima Kilimanjaro

KATIKA kukabiliana na tatizo la kupotea kwa vilele vya barafu katika Mlima Kilimanjaro, kunakosababishwa na ongezeko la joto duniani na mabadiliko ya tabianchi, mradi wa The Kilimanjaro umetangaza kushirikiana na mradi wa Trees4Kili kupanda miti milioni moja.

Mwenyekiti wa Mfuko wa Taifa wa Dhamana ya Hifadhi ya Mazingira (NETF), Ali Mufuruki.

Kazi ya upandaji miti inatarajiwa kufanyika Aprili 23, mwakani kwa lengo la kufidia milioni ya miti inayokatwa kila mwaka katika mkoa wa Kilimanjaro kwa shughuli za kuni.

 

Mwenyekiti wa Mfuko wa Taifa wa Dhamana ya Hifadhi ya Mazingira (NETF), Ali Mufuruki, akizungumza uzinduzi wa mradio huo, uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana, alisema nchini zaidi ya hekari 300,000 za miti hukatwa kila mwaka.

“Kwa ushirikiano na wadau wa mazingira mkoani Kilimanjaro, mradi huu utazindua mpango wa kupanda miti wenye lengo la kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kurejesha misitu kwa kupanda miti milioni moja kila mwaka kwenye tukio la kupanda miti litakalokuwa linafanyika kila mwaka,” alisema.

 

Kadhalika alisema mradi huo utawawezesha wakazi wa jamii zinazozunguka Mlima Kilimanjaro kupanda na kutunza miti katika maeneo yaliyoathirika, kuelimisha vizazi vijavyo vilivyo shuleni kuhusu utunzaji wa mazingira na kubadilisha tabia kupitia ushiriki kamilifu katika shughuli za upandaji miti, usimamizi na ufuatiliaji wa ukuaji wa miti hiyo kupitia teknolojia ya simu za mkononi.

Alisema zaidi ya asilimia 90 ya Watanzania hutumia mkaa na kuni kwa ajili ya kupikia na kupata nishati ya mwanga, na hii inatarajiwa kuongezeka kulingana na ongezeko la idadi ya watu.

“Hii inaleta changamoto kubwa katika kupambana na kasi ya ukuaji wa ukataji wa misitu ambao unaendelea nchini. Huu ni wakati wa kushirikiana,” alisisitiza Mufuruki.

Pia alihimiza wadau kuchukua hatua endelevu katika kupambana na ukataji wa misitu na kwamba hatari ya uharibifu wa mazingira itavikumba vizazi vijavyo.

 

 

 

Habari Kubwa