Mikataba gesi, uvuvi kufumuliwa

18Nov 2017
Sanula Athanas
Nipashe
Mikataba gesi, uvuvi kufumuliwa

BAADA ya kukabidhi serikalini ripoti ya uchunguzi wa makinikia ya almasi na tanzanite, Bunge limeunda tena kamati mbili, safari hii kuzichunguza kwa mwezi mmoja sekta za uvuvi wa bahari na gesi.

Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Uchunguzi huo unatarajiwa kuja na pendekezo la kufumua mikataba ya gesi na leseni za uvuvi wa meli zinazovua bahari kuu kutokana na uongozi wa bunge kuweka bayana kwamba nchi hainufaiki ipasavyo na rasilimali yake hiyo.

Julai 5, Spika wa Bunge, Job Ndugai alitangaza kuunda kamati mbili za kuchunguza na kuishauri serikali kuhusu uchimbaji na biashara ya madini ya almasi na tanzanite na ripoti zake zilikabidhiwa kwa Rais John Magufuli miezi miwili baadaye.

Wakati serikali inaendelea kufanyia kazi mapendekezo ya kamati hizo, Spika Ndugai, katika kikao cha mwisho cha mkutano wa tisa wa Bunge la 11 jana, alitangaza tena kuwa ameunda kamati nyingine mbili zitakazoshughulikia uvuvi wa bahari kuu na gesi akisisitiza kuwa lazima chombo hicho cha kutunga sheria kijue kwanini sekta hizo hazichangii Pato la Taifa.

Katika kamati hizo mbili mpya, Spika Ndugai amewajumuisha tena Mbunge wa Bukombe, Dotto Biteko, aliyekuwa mwenyekiti wa kamati iliyochunguza uchimbaji na biashara ya tanzanite pamoja na Mussa Zungu, aliyekuwa mwenyekiti wa kamati iliyochunguza almasi.

Akitangaza kuunda kamati hizo jana, Spika alisema ametumia Kanuni ya 5 (1) cha Kanuni za Kudumu za Bunge toleo la Januari 2016 ambacho kinampa madaraka ya kuunda kamati kwa kadri atakavyoona inafaa.

Kiongozi huyo wa Bunge alisema kumekuwa na hali ya kusuasua katika sekta hizo, akibainisha kuwa uvuvi wa bahari kuu unachangia Pato la Taifa kwa asilimia 1.4 ambayo ni sawa na Sh, bilioni 3.2 kwa mwaka wakati kuna zaidi ya Sh. bilioni 400 ambazo zinapotea bure.

Alisema ukubwa wa ukanda wa bahari katika uvuvi wa Tanzania unalingana na nchi ya Namibia ambayo yenyewe inaingiza pato kwa asilimia 10, hivyo kuna kila sababu ya kupitia upya sekta hiyo ikiwamo kuangalia mirabaha ya leseni za uvuvi wa meli zinazovua bahari kuu.

Ndugai aliwataja wajumbe 11 wanaounda kamati ya kuchunguza uvuvi wa bahari kuu kuwa ni pamoja na Zungu, Salum Mwinyi Rehani, Masoud Salim Abdallah, Tauhida Nyimbo, na Mbaraka Dau.

Alisema wengine ni Dk. Immaculate Semesi, Dk. Christina Ishengoma, Stanslaus Mabula, Mussa Mbarouk, Cosato Chuma na Anastazia Wambura ambaye ni mwenyekiti wa kamati hiyo.

Spika Ndugai aliwataja wajumbe watakaochunguza gesi kuwa ni pamoja na Innocent Bashungwa, Dunstan Kitandula, Dk. Seleman Yusufu, Wanu Hafidhi Ameir, Oscar Mukasa na Ruth Mollel.

Alisema wengine ni Richard Mbogo, Omari Kigua,Abdallah Mtolea, Sebastian Kapufi na Biteko ambaye atakuwa mwenyekiti.

Ndugai alisema Ofisi ya Katibu wa Bunge ndiyo itaangalia namna ya kuwawezesha wabunge hao ili waanze kazi ndani ya siku 30 kuanzia siku ambayo ofisi hiyo itaona inafaa.

Habari Kubwa