Mbunge ahoji sababu wanaume kupendelewa

23May 2019
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Mbunge ahoji sababu wanaume kupendelewa

MBUNGE wa Ulanga Mashariki, Goodluck Mlinga (CCM), amehoji bungeni sababu za serikali kuwajali wanaume kwa kuwapa kondomu huku ikisita kutoa bure taulo za kike kwa ajili ya wanafunzi.

Mlinga alihoji suala hilo bungeni jijini Dodoma jana, baada ya kumalizika kwa kipindi cha 'Maswali', akieleza kuwa takwimu za wanafunzi kufanya vibaya darasani ni mbaya kwa wanafunzi wa kike hasa wanaotoka maeneo ya vijijini.

Alisema anaona sababu kubwa ya kufeli kwa wanafunzi wa kike katika maeneo hayo ni kutohudhuria shuleni kipindi wanapokuwa katika siku zao za hedhi.

"Mheshimiwa Spika, Bunge limekuwa likipiga kelele sana serikali namna gani itawasaidia wanafunzi kwa kuwapa taulo za kike bure.

"Lakini Mheshimiwa Spika, tumeshuhudia serikali ina utaratibu wa kutoa vifaa tiba kwa makundi mbalimbali ya wananchi wake ili kuwasaidia kuepukana na magonjwa mbalimbali katika kuboresha afya.

"Kwa mfano, Mheshimiwa Spika, tumeona serikali inatoa bure ARVs (dawa za kupunguza makali ya Virusi vya Ukimwi) bure kwa watu wanaoishi na VVU (Virusi vya Ukimwi), wagonjwa wa kifafa wanapewa dawa bure, TB (kifua kikuu) wanapewa dawa bure.

"Hata ... (alitaja jina la dawa inayoaminika inatibu ugonjwa wa malaria) ilitakiwa iuzwe Sh. 20,000, lakini inauzwa Sh. 2,000. Mheshimiwa Spika, serikali inagawa mipira ya kiume bure hadi kwenye zahanati za vijijini.

"Mheshimiwa Spika, kweli serikali yetu inatoa kipaumbele kwa wazinifu, inaacha wanafunzi! Kwanini serikali isitoe taulo za kike bure kwa wanafunzi wetu?" Mlinga alihoji. 

Spika Ndugai aliyekuwa anaongoza kikao cha jana, aliitaka serikali kuichukua hoja hiyo na kuangalia namna ya kuifanyia kazi suala hilo.

"Hilo nalo pia limefika serikalini na kwa wakati mwafaka, serikali itaona namna gani ya kuzungumza na Bunge kuhusiana na mambo haya," Spika Ndugai alisema.

Kwa muda mrefu Mbunge wa Viti Maalum, Upendo Peneza (Chadema), amekuwa akihoji bungeni kuhusu serikali kutoa taulo za kike kwa wanafunzi bila malipo.

Habari Kubwa