Mbowe afichua ya wabunge, madiwani kuhama Chadema

20Dec 2017
Romana Mallya
Nipashe
Mbowe afichua ya wabunge, madiwani kuhama Chadema

KIONGOZI wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, amesema wabunge wanaokimbilia Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanafanya hivyo kwa kuwa huko kuna maslahi na kwamba wana haki ya kufanya hivyo kwa sababu upinzani hauwezi kuwazuia.

Kauli ya Mbowe imetolewa ikiwa siku moja tangu kutolewa taarifa katika Mkutano Mkuu wa Tisa wa CCM kuwa kuna mbunge na madiwani wanane kutoka upinzani ambao wanamwomba Mwenyekiti wa chama hicho, Rais John Magufuli,  kuhamia CCM.

Akifungua mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete, Rais Magufuli alisema kwa sasa kuna watu wengi wanaorejea CCM kutoka upinzani na wengine wanaojiunga na chama hicho kwa mara ya kwanza.

“Kuna mbunge ananiomba sana anataka kuhamia na madiwani wanane… Hiki kimbunga na (wapinzani) wataisoma namba,” alisema Mwenyekiti huyo bila kuweka hadharani jina la mbunge huyo.

Alipoulizwa jana kuhusu msimamo wa upinzani dhidi ya wimbi la wabunge wa upinzani kukimbilia CCM, Mbowe alisema “Mtu kama hakusaidii ana faida gani na wewe?...waache wahame, mtu anapokulilia shida na wewe unakuwa msikivu, anaponunuliwa mwache aende, si walikuwa huko huko, waache aende wanafahamu siri za kwao.”

“Kwa mwaka mtu unachukua mshahara na posho Sh. bilioni moja na pointi unakuja unaacha pengo kwenye jimbo. Watatuma tena bilioni moja na pointi kwenye jimbo, watasema wewe si una hela tumia hela yako,” alisema.

Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alidai kuwa wao (chama tawala) wanatumia fedha, lakini upinzani wanatumia nguvu kutetea wananchi.

“Wao kwa sababu wameshikilia kila kitu waache wafanye wanavyotaka. Hatumzuii mtu kuhama chama, anahama chama anakwenda kwenye maslahi,” alisema.

Aidha, Mbowe alisema CCM walisema ifikapo mwaka 2020 upinzani hautakuwapo, hivyo wanafanya hivyo kutimiza ndoto yao.

“Lakini ngoja nikuambie, upinzani tutaendelea kuwapo na tutaendelea zaidi kuwapo. Serikali bila upinzani haiwezi kuitwa serikali, ndiyo maana ya demokrasia. Hata  Kenya hawajasimamia sehemu moja. Ifikapo sehemu fulani tutamwapisha mtu fulani,” alisema.

Katika mkutano wa Dodoma, Rais Magufuli alisema kabla ya kupokewa hufanyiwa tathmini ili chama hicho kisije kuchukua mamluki.

Hamahama ya wabunge ilianza Oktoba 30, mwaka huu, baada ya Lazaro Nyalandu (45), aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki tangu mwaka 2000, kujiuzulu kwa madai ya kukosekana kwa demokrasia ya kutosha ndani ya CCM, miongoni mwa sababu kadhaa. Aliomba na kujiunga na Chadema tangu hapo.

Desemba 2, aliyekuwa Mbunge wa Kinondoni kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Maulid Mtulia, alitangaza kujiuzulu ubunge, kujivua uanachama na kuhamia CCM.

Mtulia alisema katika taarifa yake kuwa: “Nimebaini kuwa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho ni chama tawala inafanya kazi kubwa ya kutekeleza Ilani na imefanya vizuri katika mambo mengi ambayo sisi upinzani tuliahidi kuyatekeleza.”

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Mbunge wa Siha (Chadema), Dk. Godwin Mollel, naye alitangaza kujiuzulu nafasi yake ya ubunge na kujiunga na CCM kwa kile alichodai  kumuunga mkono Rais Magufuli. 

Mbali na wabunge hao, John Mnyika wa Chadema (Ubungo), naye ametajwa tajwa kutaka kuhamia CCM lakini akakanusha. Halmashauri ya Ubungo inaongozwa na Chadema. 

Habari Kubwa