Mauaji tena Kibiti

19May 2017
Na Waandishi Wetu
Nipashe
Mauaji tena Kibiti
  • Sasa yamkumba mwenyekiti mstaafu CCM wilaya, Polisi wataja kinachowakwamisha...

MATUKIO ya kuuawa mara kwa mara kwa wananchi wasio na hatia katika Wilaya ya Kibiti, mkoani Pwani, yameendelea tena baada ya kuuawa kwa kupigwa risasi mwenyekiti wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo, Iddy Kirungi (60).

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga.

Mauaji hayo ambayo huwakuta zaidi viongozi wa serikali za vijiji na wale wa CCM, yameshagharimu maisha ya takribani watu 30 na kuzidisha hofu kwa wakazi wa wilaya hiyo.

Aidha, licha ya Jeshi la Polisi kuendesha operesheni kadhaa za kuwasaka wahalifu ikiwamo kuiweka wilaya ya Kibiti katika orodha ya maeneo yanayounda Mkoa mpya wa Kipolisi, bado mambo yanaelekea kuwa magumu kutokana na kile kinachoelezwa na Polisi kuwa ni kutokuwapo kwa ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wananchi katika kuwapatia taarifa muhimu za kukomesha vitendo hivyo.

Kwa mujibu wa polisi, tukio hilo la kuuawa kwa kiongozi huyo wa zamani wa CCM lilitokea juzi saa 1:40 usiku katika kijiji cha Muyui, Kata ya Mtunda wilayani humo.

Akizungumza na Nipashe jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga, alisema watu wasiofahamika walimpiga risasi ya bega la kulia Kirungi wakati akitoka bafuni nje ya nyumba yake.

Alisema katika tukio hilo, watuhumiwa hao walimjeruhi tumboni kwa risasi mtoto wa marehemu, Nurdin Kirungi (18), ambaye sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Mchukwi.

Alisema baada ya tukio hilo, watu hao walitokomea kusikojulikana na kwamba hakuna anayeshikiliwa kufuatia tukio hilo.

Kamanda Lyanga alitoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwao ili kuwafichua wale wote wanaojihusisha na vitendo vya mauaji huku pia akiwataka kuchukua tahadhari binafsi za kiusalama, hasa nyakati za usiku.

CHANZO KUENDELEA MAUAJI
Kamanda Lyanga alipoulizwa maendeleo ya operesheni wanayoifanya kila uchao kwa sasa ili kuwatia mbaroni wauaji na kuwafikisha mbele ya mkono wa sheria, alisema wamekuwa wakipata wakati mgumu kwa kukwamishwa na changamoto ya kukosekana kwa taarifa muhimu kutoka kwa wananchi wa maeneo hayo.

“Kikubwa kwetu ni taarifa ili tuweze kuzifanyia kazi. Wananchi wanagoma kutoa ushirikiano kwetu kwa hiyo na sisi inatuwia vigumu kutambua yupi ni mhalifu na yupi siyo mhalifu,” alisema.

“Wahalifu wanaishi nao huko vijijini. Kuna watu miongoni mwao wanashirikiana na wahalifu hao. Sisi hatuwajui. Linapotokea tukio, ukiwafuata wananchi ili watupe ushirikiano hawataki.

“Matukio yanatokea, watu wanakufa, tunafanya operesheni, lakini sasa tunakamata na kuwaachia watu kwa sababu hatuna ushahidi wa kujitosheleza ambao wananchi wa eneo husika ndiyo wanao,” alisema na kuongeza:

“Ushahidi tunaokuwa nao sisi ni wa kimazingira, ambao kiupelelezi hausaidii sana... huwezi kumkamata mtu kwa kumhisi halafu kesho ikabainika siyo jambazi… kufanya hivyo ni kulichafua Jeshi la Polisi,” alisema.
 
MAUAJI KABLA YA JUZI
Wakati polisi wakikiri kukwamishwa na ukosefu wa taarifa muhimu za kuwakabili wahalifu, taarifa zinaonyesha kuwa tukio la juzi limesababisha umauti kwa mtu wa 30 asiye na hatia, idadi inayohusisha matukio ya kuanzia mwaka jana. Mbali na viongozi, wengine waliopoteza maisha yao ni raia wa kawaida na askari polisi.

Baadhi ya matukio ya mwaka jana ni pamoja na kuuawa kwa kupigwa risasi mwenyekiti wa kijiji cha Nyambunga, Saidi Mbwana.

Oktoba mwaka jana, aliuawa Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Nyambuga, Ally Milandu, ambaye alivamiwa na watu wanne waliomshambulia kwa kumpiga risasi.
Novemba, wenyeviti wawili wa vitongoji wa kijiji cha Nyambunda waliuawa kwa kupigwa risasi.

Aidha, matukio mengine ni pamoja na lile lililotokea Januari mwaka huu katika kijiji cha Nyambunga, kitongoji cha Mkwandara alipouawa mfanyabiashara Oswald Mrope, kwa kupigwa risasi mbele ya familia yake.

Februari mwaka huu yalitokea matukio mawili, la kwanza majambazi walivamia nyumba ya mwenyekiti wa kijiji cha Jaribu, Bakari Msanga ambaye alifanikiwa kutoroka, lakini wahalifu hao walirejea na kuimwagia mafuta nyumba yake na kuichoma moto.

Tukio la pili katika mwezi huo ni lile la mauaji ya Ofisa Upelelezi wa Wilaya ya Kibiti (OC-CID), Peter Kubezya na Ofisa wa Misitu ambaye alikuwa Mkaguzi wa Kituo cha Ukusanyaji mapato ya ushuru katika Kijiji cha Jaribu, Peter Kitundu na pia mlinzi Rashid Mgamba. Wote waliuawa kwa kupigwa risasi.

Machi, Polisi waliwaua watu watatu katika Daraja la Mkapa waliokuwa wakijaribu kukwepa vizuizi vitatu vya barabara wakiwa na pikipiki.

Mwezi uliopita, askari nane waliokuwa kwenye gari la polisi wakitoka kubadilishana lindo na wenzao walipofika eneo la Mkengeni, Kata ya Mjawa wilaya ya Kibiti, waliuawa na watu hao kwa kupigwa risasi. Katika tukio hilo, askari mmoja alijeruhiwa na muda mfupi baada ya tukio hilo, Polisi walitangaza kuwaua watuhumiwa wanne baada ya kudaiwa kuwa walibaini maficho ya muda ya majambazi hao.

Mwezi huu peke yake, waliofariki ni pamoja na kada wa CCM Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani, Amir Chanjale na aliyekuwa Katibu wa chama hicho, Kata ya Bungu wilayani Kibiti, Arife Mtulia. Wote waliuawa pia kwa mashambulizi ya risasi kutoka kwa watu wasiojulikana.
 
MADIWANI WATISHIKA
Matukio ya mauaji ya mara kwa mara katika wilaya ya Kibiti yamewatisha madiwani na kuitaka halmashauri ya wilaya yao kuwapatia vitambulisho maalumu vya utambuzi.

Katika ombi lao walilolitoa kwa mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo, Alvera Ndabagoya, baadhi ya madiwani walidai kuwa hivi sasa, kuna tishio la kiusalama na hivyo, ni vyema wakapatiwa vitambulisho ili watambulike kirahisi na hivyo kuepukana na athari za operesheni mbalimbali za kuimarisha amani na utulivu katika maeneo yao.

Katika majibu yake, Ndabagoya alikubaliana na hoja hiyo na kuwaambia kuwa analishughulikia ili ifikapo mwezi ujao kila diwani awe na kitambulisho.

'Tulishindwa kutengeneza vitambulisho kutokana na mtengenezaji wa kwanza kutuambia kitambulisho kimoja kitatengenezwa kwa Sh. 14,000. Lakini baada ya kumtafuta mtengenezaji mwingine, tumefanikiwa kutengenezewa kwa Sh. 4,000 kwa kila kitambulisho kimoja,” alisema Ndabagoya.

*Imeandikwa na Romana Malya (Dar) na Yasmine Protace (Kibiti).

Habari Kubwa